Mbwana Ally Samatta Mtanzania anayecheza katika klabu ya Genk ya Nchini Ubelgiji jana jumapili ameisaidia timu yake kutinga katika michuano ya Europa Msimu ujao.
Genk iliibuka na ushindi wa magoli 5 - 1 dhidi ya Sporting Charleroi. Katika mchezo huo Samatta alifunga goli katika dakika ya 27, goli la pili kwa upande wa Genk. Nyota wa Mchezo huo alikuwa ni Nikolas Karelis aliyepiga Hat-trick, akifunga goli la kwanza kwa njia ya mkwaju wa penati baada ya Samatta kufanyiwa faulo ndani ya penati box.
Karelis alianza kufunga goli la kwanza katika dakika ya 17 ya mchezo kisha Samatta akatupia la pili dakika ya 27, akafuata Sandy aliyezamisha wavuni goli la tatu mnamo dakika ya 45, hivyo kuifanya Genk kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa goli 3.
Karelis ambaye aliisumbua ngome ya ulinzi ya Sporting katika mchezo huo alifunga goli la 4 kunako dakika ya 56 ya mchezo na baadae dakika ya 71 akafunga goli la 5 na kukamilisha hat-trick yake.
Genk walikuwa wanahitaji ushindi wa magoli zaidi ya matatu katika mchezo huo ili kuwawezesha kusonga mbele kufuatia kufungwa 2 - 0 katika mchezo wa kwanza.
Hivyo matokeo hayo ya 5 - 1 kumewafanya Genk kufuzu kucheza michuano ya Uropa lakini wataanzia hatua ya mtoano ambapo wakifuzu ndipo wataingia katika hatua ya makundi.
0 comments:
Post a Comment