Wednesday, February 8, 2017

Manji Amcharukia Makonda

Operesheni ya kuwataja hadharani wanaotuhumiwa kujihusisha na madawa ya kulevya limechukua sura mpya baada ya leo Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mh. Paul Makonda kutaja orodha ya awamu ya pili ambayo imewahusisha watu wengi mashuhuri hapa nchini.

Katika orodha hiyo, Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji ametajwa na kutakiwa aripoti kituo cha polisi siku ya Ijumaa pamoja na watuhumiwa wengine. Wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni Mh. Freeman Mbowe (Katibu Mkuu wa Chadema), Idd Azam (Mbunge Mstaafu) pamoja na Mchungaji Gwajima.
Mara baada ya kutajwa kwa majina hayo, Mwenyekiti wa Yanga, ametokea hadharani kuonyesha hisia zake juu ya yeye kujumuishwa katika orodha hiyo na kutakiwa kwenda polisi.

Akizungumza baada ya zoezi hilo la Paul Makonda kukamilika, Manji amesema kutajwa kwake kumemchafua yeye pamoja na Yanga kwa Ujumla.

"Umenichafua mimi, na kama umenichafua mimi umeichafua Yanga nzima,na kama umeichafua Yanga maana yake watu milioni 30 wana Yanga nao umewachafua, maanake mimi kama mwenyekiti wa Yanga, aidha ni mlevi kwenye dawa za kulevya, nauza au unataka mimi nikupe taarifa,Mimi nasimamia mamilioni ya wananchi, amani na utulivu na maendeleo" alisema Yusuf Manji alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ilala jijini Dar Es salaam.

Aidha Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, yeye ataenda katika kituo cha polisi kesho Alhamisi na si Ijumaa kama ambavyo Paul Makonda alivyoagiza.

"Kwanza mimi nataka kesho niende polisi, iwe Central au itakuwa wapi, asubuhi, watataka maelezo au msaada nitawapa msaada ili hili jambo liishe" Aliongeza Manji.

Hakuishia hapo Mwenyekiti huyo, kwani aliendelea kusema kuwa, baada ya taarifa zote watakazozihitaji naye kutoa ushirikiano, ataanza mambo yake ya kufuatilia haki yake.

"Lakini baada ya hapo, nitaanza mambo yangu ya kuomba haki yangu, na vipi mtu anaweza kunitaja kwenye vyombo vya habari, kuniita mimi kwenye kituo cha polisi halafu unaniita kaka, kumbe unataka kunidhalilisha kupitia njia hiyo" alisema Manji.

0 comments:

Post a Comment