Tuesday, May 24, 2016

AZAM FC IMEKUJA KUINUA SOKA LA VIJANA TANZANIA

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeonyesha kweli imedhamiria kuinua soka la vijana nchini baada ya leo kutangaza kuandaa michuano ya vijana ya Afrika Mashariki itakayoanza kutimua vumbi kwenye viunga vya Azam Complex Juni Mosi hadi Juni 5 mwaka huu.


Kwa kuanzia mwaka huu michuano hiyo itakayojulikana kama ‘Azam Youth Cup 2016’ itahusisha timu nne pekee, za Tanzania zikiwa ni kikosi cha vijana ya Azam FC ‘Azam Academy’ na Future Stars Academy (Arusha) pamoja na timu mbili nje ya Tanzania  Ligi Ndogo Academy (Kenya) na Football for Good Academy (Uganda).

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Azam FC, Said Mohamed, alisema kuwa malengo makubwa ya michuano hiyo ni kukuza vipaji vya vijana na baadaye kupata wachezaji watakaocheza katika timu kubwa ya Azam FC ambao ndio watakuza soka.

“Moja ya madhumuni ya kuanzisha Azam FC ni kukuza soka la vijana, kwa hiyo kwa kusisitiza hilo leo tunatangaza kuandaa michuano ya vijana ya Afrika Mashariki, kutakuwa na timu kutoka Kenya, Uganda na Tanzania, wenzetu wote duniani waliopata maendeleo walianza chini huku kwa vijana na wakapanda juu, hawakuanza juu ndio wakashuka chini.

“Hivyo kuwa na timu kubwa pekee hakutoshi lazima uwe na timu za vijana ili hao vijana ndio wawe chemchem ya kuweza kupatikana maendeleo ya mpira,” alisema.

Kocha wa vijana anena

Kwa upande wake Mtaalamu wa soka la vijana wa Azam FC, Tom Legg, michuano hiyo itasaidia kuwajaribu wachezaji wake kutokana na kukosa mechi nyingi za ushindani za mara kwa mara.

“Michuano hii ya Azam Youth Cup 2016 ni maalumu kwa ajili ya vituo bora vya kukuza vipaji (academy) kuja hapa kushindana, sio tu kwa Afrika Mashariki bali na sehemu nyingine, hivyo hii ni sehemu yetu tu ya kuanzia mwaka huu na tutaanza kualika klabu nyingine zaidi na vituo vya kukuza vipaji zaidi na hii ni katika kuipanua michuano hiyo hapo baadaye.

“Kwa kweli tunafurahia sana kuzialika hapa timu kutoka Kenya, Uganda na Arusha, hii itakuwa ni nzuri kwa wachezaji wetu kwani walikosa mechi nyingi za ushindani za mara kwa mara, tumecheza mechi nyingi za U-20 na timu za vijana za Ligi Kuu, lakini kwa sasa tutapata mechi nzuri zaidi za kuwajaribu wachezaji wetu,” alisema.

Legg aliwaomba mashabiki kujitokeza kushuhudia mechi hizo huku akidai itakapoanza michuano hiyo watapata fursa ya kushuhudia mechi mbili kwa siku zitakazoanza saa 10.00 jioni na ya pili ikipigwa saa 1.00 usiku ndani ya Uwanja wa Azam Complex.

Kocha huyo raia wa Uingereza, aliongeza kuwa michuano hiyo itaendeshwa kwa mfumo wa ligi na bingwa atakuwa ni yule aliyekusanya pointi nyingi kutokana na mechi alizocheza.

C.E.O Azam FC aichambua michuano hiyo

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema kuwa michuano hiyo haijaandaliwa kwa lengo la kucheza mpira tu bali timu zote shiriki zitapata fursa ya kuingia darasani na kupeana elimu na uzoefu wa kuendesha soka la vijana kupitia mipango ya kila timu.

“Hivyo tunajifunza kutoka kwa watu wote, kwa hizo siku sita watakazokuwepo hapa tunacheza mpira siku moja, siku nyingine ya pili hakuna mpira na hiyo siku ambayo kutakuwa hamna mpira ndio siku ya kuingia darasani, watu wote tunasoma wachezaji wanasoma na viongozi wanasoma, mwisho wa siku sote tunakuwa tumepata kitu fulani,” alisema.

Kawemba pia alitolewa ufafanuzi kwanini wamechukua vituo vya kulea vipaji (academy) na sio timu zenye majina makubwa, ambapo alisema: “Watu walitegemea tuichague timu ya vijana ya Gor Mahia, timu ya vijana ya Villa, lakini tulifanya utafiti wetu na kwenda kwenye academy zinazofanya vizuri na sisi tukitaka kuipeleka academy yetu huko, hivyo academy zinazokuja hapa ndio bora katika nchi husika.”

Alisema kuwa mwezi Desemba mwaka huu Azam FC itakuja na kitu kikubwa zaidi ya hicho, ambapo zitashiriki timu za hadhi nyingine nje ya ukanda wa Afrika Mashariki na hata nje ya Afrika lengo likiwa ni kupata uzoefu tofauti wa uendeshaji wa soka la vijana.

“Hii ni changamoto mpya na ujumbe tunaowapa Watanzania na timu nyingine zote ni kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya leseni ya klabu (Club Licencing), sasa Azam FC hatutaki tufike wakati tuulizwe hapana hilo ni jukumu ya kila klabu, vilabu vya hapa nyumbani vikishaingia kwenye Club Licencing mashindano kama haya watafaidika nayo, lakini wasipoingia tutaendelea kutoka nje na kuzialika timu zilizoingia kwenye mfumo huu,” alisema.

Kawemba alichukua fursa hiyo kuwakaribisha watu wengine wanaoendesha academy zinazotambulika kwa anuani nchini, kujiunga kwenye mafunzo yatakayokuwa yakitolewa wakati mashindano hayo yatakapokuwa yakiendelea huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa bure na hakuna gharama zozote.

Aliongeza kuwa timu shiriki zitaanza kuwasili kuanzia Mei 29 na 30 mwaka huu na zitafikia katika Hosteli za Azam Complex, ambapo hakuna timu itakayoruhusiwa kutoka nje wakati michuano hiyo ikiwa inaendelea isipokuwa Juni 4 watakapokwenda kushuhudia mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Misri utakaofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

“Michuano hiyo inahusisha vijana wadogo na hivyo tunasema wazi kabisa ya kuwa waamuzi watakaochezesha nao watakuwa ni vijana wadogo, ambapo mechi zote zitaonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni kupitia kingamuzi cha Azam TV na muda ni rafiki, lakini kwa wakazi wa Mbagala itakuwa ni vizuri kuja uwanjani na kushuhudia,” alisema.

Kawemba alimalizia kwa kusema kuwa kutakuwa na tuzo maalumu kwa vijana waliofanya vizuri, ambazo ni Kombe kwa aliyeibuka bingwa, pia kuna tuzo za mtu mmoja mmoja za Kipa Bora, Beki Bora, Kiungo Bora, Mshambuliaji Bora, Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa mashindano hayo, wote watapatikana kupitia uchambuzi maalumu utakaokuwa ukifanywa na makocha watakokuwa wakishuhudia mechi hizo.

RATIBA KAMILI

Juni 1, 2016

10.00 Jioni - Azam vs Future Stars

1.00 Usiku - FFG vs Ligi Ndogo

Juni 3, 2016

10.00 Jioni - Ligi Ndogo vs Future Stars

1.00 Usiku - Azam vs FFG

Juni 5, 2016

10.00 Jioni - FFG vs Future Stars

1.00 Usiku - Azam vs Ligi Ndogo

CHANZO: AZAM FC

0 comments:

Post a Comment