Wachezaji Juma Abdul na Salum Telela wataikosa mechi kati ya Yanga na Mo Bejaia, mechi ya kwanza katika hatua ya makundi kombe la shirikisho CAF.
Telela na Juma Abdul hawatakuwepo katika kikosi kitakachoenda nchini Uturuki kwa kambi ya siku Tano kujiandaa na mchezo wao wa kombe la shirikisho la soka Afrika (CAF CC) dhidi ya Mo Bejaia ya nchini Algeria. Kwa mujibu wa Meneja wa Yanga Hafidh Saleh, Juma Abdul ataikosa mechi hiyo kwa sababu ni majeruhi wakati Telela yeye mkataba wake umemalizika klabuni hapo na uongozi wa timu mpaka sasa haujamuongezea mkataba mpya.
"Juma Abdul ni majeruhi, hivyo hatoweza kwenda, Telela yeye mkataba wake umeisha na mpaka sasa uongozi bado haujamuongezea" alisema Hafidh Saleh.
Aidha wachezaji wapya wa timu hiyo, ambao ni Hassan Kessy, Andrew Vicent, Juma Mahadhi na Beno Kakolanya watakuwa ni miongoni mwa watakaokuwepo katika msafara huo.
Inadaiwa kuwa Telela ameshafanya mazungumzo na timu za Simba na Azam kwa nia ya kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Saleh amesema mara baada ya mchezo wao na MO Bejaia watarejea Uturuki kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo utakaofanyika uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam na watarejea nchini siki mbili kabla ya mchezo huo.
0 comments:
Post a Comment