Monday, June 13, 2016

GOLI LA UTATA LAITUPA BRAZIL NJE YA COPA AMERICA

Kwa Mara ya kwanza tangu mwaka 1987 Brazil inatolewa katika hatua ya makundi michuano ya Copa America.

Timu ya Taifa ya Brazil imeondolewa katika michuano ya Copa America kufuatia goli la utata lililofungwa na Ruidiaz kunako dakika ya 75'.

Raul Ruidiaz alionekana kuunawa mpira kabla hajafunga goli hilo ambalo mwamuzi wa mchezo huo aliamuru mpira upelekwe kati na kuwafanya Peru kusonga mbele kutokana na ushindi huo wa goli 1 - 0.

Baada ya goli hilo Brazil walionekana kupambana bila mafanikio licha ya ukweli kuwa wameonyesha kiwango kibovu katika michuano hiyo.

Katika mechi hiyo Brazil walikuwa wanahitaji sare yoyote ili waweze kutinga hatua ya robo fainali.
Wachezaji wa Brazil walimsongasonga mwamuzi wa mchezo huo wakilipinga goli hilo lakini tayari mwamuzi alishalikubali goli hilo.
Kutokana na kusongwa sana na wachezaji wa Brazil Cunha ilibidi awasiliane na mshika kibendera ili kupata uhakika wa goli hilo.

Baada ya dakika takribani nne mpira ukiwa umesimama wachezaji wa timu zote wakimsonga songa mwamuzi hatimaye mwamuzi huyo aliamuru mpira uendelee na kwamba hilo goli lilikuwa ni halali, lakini picha za marejeo kutoka katika pembe mbalimbali zilionyesha wazi kuwa Ruidiaz aliucheza mpira huo kwa mkono na kuuzamisha wavuni.

Kwa matokeo hayo sasa Peru watacheza na Colombia katika hatua ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi B.

Kocha wa Brazil, Dunga aliyalaani maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo kwa kitendo chake cha kukubali goli hilo.

"Nina hakika mashabiki wa Brazil wameuona mchezo na wameona jinsi gani Brazil walivyotolewa, Timu haijatolewa kwa kushindwa kucheza mpira" alisema Dunga.

"Nashindwa kuelewa ni nani na nini mwamuzi alikuwa anawasiliana nae, ni wazi kuwa mchezaji wa Peru aliucheza mpira kwa mkono" alisema Dunga ambaye aliongeza kuwa yeye pia ameangalia picha za marudio na kuona wazi kuwa goli hilo lilifungwa kwa mkono.

Safari ya Wabrazil kusahau
aibu yao ya kipigo cha goli 7 kwa 1 walichokipata katika michuano ya kombe la dunia imefika ukingoni katika michuano hiyo ya Copa America Contenario 2016.
==============
 Bonyeza hapa ku-Like Page yetu ya Facebook
==============

0 comments:

Post a Comment