Friday, June 10, 2016

AARON NYANDA AJIENGUA UCHAGUZI YANGA

Nyanda aliyekuwa anagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, amejitoa kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika kesho Juni 11, 2016.


Nyanda ambaye alichukua fomu za kuwania nafasi hiyo kwenye ofisi za shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania (TFF) amesema ameamua kujitoa kwa sababu muda uliobaki kufanya kampeni ni mfupi, tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo ikiwa ni kesho Juni 11.

"Nimeamua kujitoa kwa vile muda ni mchache tofauti na mchakato ule ambao TFF waliutangaza awali, Huku ukiangalia muda umeisha kesho (leo) mwisho wa kampeni, sasa utafanyaje kampeni ya siku moja bila kujipanga, ndio maana nimeamua kukaa pembeni nipishe msongamano" alisema Aaron Nyanda.

Nyanda amefikia hatua hiyo baada ya kamati ya uchaguzi Yanga kutangaza kuwa wagombea wote waliochukua fomu katika ofisi za shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, kutakiwa kuchukua tena fomu hizo katika makao makuu ya klabu ya Yanga kwa kile walichodai kuwa hawana uhakika kama wote waliochukua fomu hizo TFF ni wanachama halali wa Yanga.

Katibu mkuu wa kamati ya Uchaguzi Yanga, Bakili Makele amesema wagombea wote waliojitoa wamerudishiwa fedha zao huku wale walioamua kuendelea na mchakato kutakiwa kujaza fomu upya na kufanyiwa usaili.

Wakati Nyanda akitangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho, mgombea mwingine wa nafasi hiyo aliyekuwa amechukua fomu TFF, Tito Osoro amesema yeye atapambana hadi dakika ya mwisho, Tito tayari alishafanyiwa usaili na kuruhusiwa kuendelea na kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo.

Wagombea wengine waliochukua fomu TFF na kulazimika kuchukua tena Yanga na kufanyiwa usaili ni; Edgar Chibura, Ramadhani Kampira, Paschal Laizer na Bakari Malima "Jembe Ulaya"


0 comments:

Post a Comment