Sunday, May 1, 2016

HIZI NDO REKODI ZA SIMBA NA AZAM (HEAD-TO-HEAD)


Simba leo wataingia uwanjani kuwakabili Azam Fc vijana wa Chamanzi katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara. Timu hizi zinakutana leo zote zikiwa zinahitaji matokeo ya ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupigania ubingwa wa ligi kuu. Katika kujiandaa na mchezo huo Simba wao walielekea Visiwani Zanzibar kwenda kujiweka fiti huku Azam wakiwa katika michezo ya kombe la FA. 

Siku za hivi karibuni timu zote Simba na Azam FC hazijawa na muendelezo Mzuri wa kushinda katika mechi zao kwani Simba wametoka kufungwa na Toto katika mechi ya ligi na walifungwa pia na Coastal katika mchezo war robo fainali ya kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).  Wakati Azam Fc wametoka kumfunga Majimaji magoli 2-0 baada ya kumfunga Mtibwa goli 1-0, na mechi yao waliyoshinda kwa mikwaju ya penati walipocheza na Mwadui Fc katika mechi ya nusu fainali ya kombe la FA.

Simba inashika nafasi ya 3 katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 57 katika michezo 25 waliyocheza wakati Azam Fc wao wanashika nafasi ya 2 kwa pointi 58 katika michezo 25 waliyocheza hadi hivi sasa.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho jana asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa ushindi kwao ni jambo muhimu kesho kama wanataka kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

“Kama mchezo huo utakuwa sare basi haitakuwa nzuri kwetu sisi na Simba katika mbio za kutwaa ubingwa, kama tunataka nafasi ya pili basi ni nzuri, lakini sisi hatutaki nafasi ya pili tunataka nafasi ya kwanza, hivyo lazima tushinde na hata wachezaji wana morali hiyo na kutambua hilo, kwani sare itampa nafasi Yanga kujihakikishia ubingwa,” alisema Hall

Kocha Hall amefurahia kurejea kwa mshambuliaji wake mahiri Kipre Tchetche pia akisisitiza kuwa katika mechi ya leo atamwanzisha nahodha wake John Bocco na Ramadhani Singano aliye katika kiwango bora kabisa kwa sasa.

Kocha Jackson Mayanja wa Simba, amekuwa akijitapa kuimarika kwa kikosi chake ambacho wiki mbili zilizopita kilifanya vibaya kwenye michuano ya kombe la FA, na hata mchezo wa ligi uliopita lakini baada ya kambi ya wiki moja visiwani Zanzibar sasa anasema wapo tayari kupambana

“Kambi yetu ya Zanzibar imekwenda vizuri na hadi tunamaliza hatuna mchezaji aliyekuwa majeruhi hivyo nifaida kwetu kuhakikisha tunaitumia vizuri ili kupata ushindi,”amesema Mayanja.

REKODI ZAO SIMBA NA AZAM FC

Timu hizo  zimekwishacheza mechi 25 kila mmoja msimu huu, Simba ikishinda 18, sare tatu na kupigwa mara nne, , Azam FC imeshinda mechi 17 kati ya hizo, ikitoa sare saba na kufungwa mmoja. Zote zimefunga jumla ya mabao 43 kila mmoja, lakini Azam FC imeruhusu mabao 16 Simba 14.
Mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya 2 – 2, magoli ya Azam Fc yakifungwa na nahodha John Bocco na yale ya samba yakipachikwa na Ibrahim Ajib.
Kihistoria timu hizo zimekutana mara 15 kwenye ligi, Azam imeshinda mara nne, Simba mara saba na mechi nne zimeisha kwa sare.





Pata habari za michezo kwa haraka zaidi kupitia soka24.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment