Wapenzi na Mashabiki wa soka kote ulimwenguni macho na masikio yao yamekaa tayari kusikia na kuona muda wowote Jose Mourinho akitangazwa kuwa kocha Mkuu wa Manchester United.
Mastaa mbalimbali wametoa mawazo yao kuhusu Mourinho mara akishapewa mikoba ya kuinoa United, wengi wamesema mengi kuhusu hilo ila Zlatan Ibrahimovic ambae pia anahusishwa na kujiunga na United amezungumza nae kuhusu maoni yake juu ya Mourinho United.
Ibrahimovic amesema kwake yeye anaamini ni usajili mzuri na utakaoleta tija kwa United, huku akisema kuwa kama unahitaji ushindi basi Mourinho ni mtu sahihi.
"Naamini Mourinho ni mtu sahihi kuirudisha United kileleni, ndio, kote alikoenda ameshinda. Anajua anachokifanya. Kama unahitaji ushindi, mchukue Mourinho" yalikuwa maneno ya Zlatan akionyesha kumkubali kwake Mourinho.
"Nilikuwa na wakati mzuri nilipokuwa nafanya kazi chini ya Mourinho. Nilipoondoka Inter nilimwambia tumekuwa na muda mfupi sana pamoja lakini ni muda wenye mafanikio makubwa na kama tutafanya tena kazi pamoja, sijui, ngoja tusubiri tuone jinsi vitu vitakavyoenda" aliongeza Ibrahimovic.
Ibrahimovic alikiri pia kuwasiliana na Mourinho mara kwa mara tangu alipoondoka Inter Milan, akisema hakuna cha kuficha, amekuwa na mahusiano mazuri sana na Mourinho na wamekuwa wakiwasiliana muda mwingi isipokuwa wiki iliyopita tu.
0 comments:
Post a Comment