Uongozi wa klabu ya Arsenal umepanga kumwongeza mkataba wa miaka 2 kocha wake Arsene Wenger mkataba ambao anatarajiwa kusaini October mwaka huu, lengo likiwa ni kupata muda wa kutosha wa kumtafuta atakaekuwa mrithi wa Wenger mara atakapoamua kuacha kibarua hicho cha kuinoa Arsenal. Mkataba wa Wenger unaishia msimu ujao, lakini kitendo cha Arsenal kushindwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kimeongeza jazba kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo huku wakitaka wenger aondoke klabuni hapo.
Wamiliki wa Arsenal wamepanga kumpa Wenger kitita kikubwa cha fedha katika msimu ujao wa usajili ili afanye usajili mkubwa ambao utaimarisha kikosi hicho wakiwa na imani kubwa kwamba kutokana na uwekezaji ambao wataufanya basi klabu hiyo inaweza kutwaa ubingwa msimu ujao.
Wenger ameiongoza Arsenal kumaliza katika nafasi nne za juu (Top Four) mara 19 na akishinda mechi yake dhidi ya Aston Villa itakuwa mara ya 20 mfululizo Arsenal kumaliza katika nafasi nne za juu chini ya uongozi wa Wenger, rekodi ambayo haijawekwa na klabu nyingine yoyote katika ligi kuu nchini England.
Licha ya kukosa taji la ligi kuu msimu huu Arsenal imefanikiwa kuwa miongoni mwa timu 5 tajiri zaidi duniani, thamani ya klabu hiyo ikipanda zaidi mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana, kitu ambacho kinawafanya wamiliki wa Arsenal kuendelea kuona umuhimu wa Wenger kuendelea kusalia katika klabu yao.
0 comments:
Post a Comment