Tuesday, April 12, 2016

Kuwaona Leicester Dhidi Ya Everton Ni Sh. Milioni 37



Klabu ya Leicester City imetangaza kiingilio cha mchezo wao dhidi ya Everton utakaopigwa kwenye uwanja wao wa nyumbani,ambapo itakuwa Euro elfu 15 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi za kitanzania milioni 37 kwa kichwa kwa watazamaji watakaonunua kwa njia ya mtandao.

Mchezo huo utafanyika tarehe 7 ya mwezi ujao,ambapo Leicester City vinara wa ligi hiyo wanatarajiwa kuonesha burudani kwani tayari watakuwa wanashangilia ubingwa kwa mara ya kwanza kama mambo yatakwenda kama yalivyo.

Uongozi wa klabu hiyo umesema tiketi zitauzwa kwa kiasi hicho cha Euro elfu 15 nje ya dakika 90 siku ya mchezo,lakini shabiki atakayehitaji ndani ya dakika hizo atalazimika kulipia kiasi cha Euro elfu 3.

Kikosi cha Leicester kimebakisha pointi 9 tu katika michezo mitano iliyosalia ili kutawazwa kuwa mabingwa wapya msimu huu,lakini bado inakabiliwa na mchuano baridi dhidi ya Tottenham inayokamata nafasi ya pili wakiwa na pointi 65 na endapo itashinda michezo yake yote mitano iliyosalia watafikisha pointi 80 wakati Leicester inahitaji kushinda michezo ili kufikisha pointi 81 kama hali itakuwa hivyo.

Michezo ya Leicester iliyo mbele yake ni dhidi ya West Ham na Swansea katika uwanja wa wa nyumbani ‘King Power Stadium’ baada ya hapo watakutana na Manchester United katika uwanja wa ‘Old Trafford, na baadaye kucheza dhidi ya Everton mchezo ambao wanategemea kutangazia ubingwa.

Tayari mashabiki wameanza kulalama kukosa tiketi za kushudia mechi zote hizo tatu zilizopo mbele,na mmoja wa viongozi wa Leicester amenukuliwa akisema malalamiko yanaweza kuongezeka kwa kuwa uwanja wao unauwezo wa kuhimilia kupokea watazamaji wasiozidi, 32,262.

Mbali na hao wanaolalamikia kukosa tiketi,wengi wao wanalalamikia kiwango kikubwa cha kiingilio wakisema ni bora ingekuwa kiwango hicho cha zaidi ya milioni 37 mtu apate tiketi mbili,ili kutoa unafuu kwa wasiokuwa na uwezo wa kukifikia.

0 comments:

Post a Comment