Thursday, April 14, 2016

Mambo 3 Ya Kujifunza Kufuatia Kichapo Cha 2 - 0 Kilichopokea Barcelona Kutoka Kwa Atletico

Mambo 3 ya kujifunza kufuatia Kichapo cha 2 – 0 ilichopokea Barcelona kutoka kwa Atletico.


1. Simeone ana kipaji cha pekee
Aliyoyafanya El Cholo huyo ( Simeone ) tangu aichukue Atletico Madrid yanatosha kutungiwa kitabu cha kumbukumbu. Ameichukua timu ikiwa inasuasua, akaijenga mwaka hadi mwaka, akaibua mastaa wapya wa soka duniani. Uwezo wake wa kuusoma mchezo na kuweka mbinu mpya dhidi ya wapinzani ni kitu kinachomuongezea heshima zaidi. Amestahili kufika nusu fainali nyingine kutokana na matunda ya kazi nzuri anayoifanya Klabuni hapo miaka mitano hivi sasa.

2. Barcelona Inaelekea Pabaya.
Mchezo wa jana ulikuwa ni wa maumivu makubwa hasa kwa wapenzi wa Barca. Louis Enrique hakuonekana mwenye wazo la nini afanye kuinusuru klabu yake, mfumo wake wa 4-3-3 Messi na Neymar wakiwa mbele haukufaa chochote. Zile pasi safi na sahihi hazikuonekana, ule ujuzi wa kina messi, suarez na Neymar kujiweka katika nafasi sahihi za kufunga magoli hazikuonekana. Sergio Busquets amepoteza pasi nyingi, Rakitic sijui alikuwa anafanya kitu gani, ma full-backs walikua ni kama hawajui majukumu yao na kubaki kukimbia kimbia tu. Na hata hao wanachama wa “MSN” yani Messi, Suarez na Neymar walipoteza heshima ya chama chao. Hii inaleta hofu ya wapi kikosi hicho kinaelekea. Sio mchezo mmoja  au miwili waliyocheza vibaya ni michezo mitano hadi sasa kutoka katika kushinda mechi 39 bila kupoteza hata moja. Kuna haja kwa Enrique kuimarisha kikosi chake.

3. Kupoteza Ubingwa Wa La Liga Kwa Barcelona Ni Kitu Cha kutegemewa Kwa Sasa.
Licha ya kuwa mbele kwa pointi 10 katika msimamo wa ligi hadi kufikia tofauti ya pointi 3 kwa sasa, hiyo haikunipa shaka na Barcelona kwani niliamini huenda wameelekeza nguvu zao zaidi kwenye Klabu Bingwa. Lakini sasa ndoto za Champions League ndo zimeshakatika baada ya kichapo cha jana, na uongozi wao katika msimamo wa ligi ni pointi 3 nyuma ya Atletico na 4 nyuma ya Real Madrid. Fainali ya Copa Del Rey ni mwezi mmoja ujao, Barcelona haitakiwi kucheza katika kiwango hiki kama wanahitaji ubingwa. Sisi mashabiki tunaamini kila kitu ni rahisi na mimi nimeishuhudia timu hii ikiidhihirishia mashabiki wake kuwa kila kitu ni rahisi kwao muda mfupi uliopita. Kwa sasa wanahitaji kujipanga upya.

0 comments:

Post a Comment