Saturday, June 3, 2017

Yote Yanayoihusu Azam FC;Usajili, Waliotemwa Wanaoingia Na Mipango Msimu Ujao

UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unapenda kuwataarifu wapenzi na mashabiki wa soka nchini kuwa imebadilisha mfumo wa usajili uliokuwa ikiutumia awali wa kusajili wachezaji kwa gharama kubwa na sasa ikijikita kwenye kufanya matumizi ya wastani pamoja na kuwatumia ipasavyo nyota watakaozalishwa kutoka kituo chao ‘Azam Academy’.


Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd, leo imeeleza kuwa kuelekea msimu ujao na kuendelea, Azam FC itaweka msisitizo na kufanya uwekezaji ipasavyo kwenye kituo chake cha kukuza vipaji ‘Azam Academy’ ili kuvuna wachezaji bora watakaopandishwa katika kikosi cha timu kubwa.

Kwa kuanzia katika kutekeleza malengo hayo, kuelekea msimu ujao Azam FC imewapandisha wachezaji sita kutoka kwenye kituo chake, ambao ni mabeki Abbas Kapombe, Abdul Haji, Godfrey Elias, kiraka Ramadhan Mohamed, kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaid, aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Daraja Kwanza (FDL) msimu uliopita kwa mabao tisa aliyofunga alipokuwa kwa mkopo Ashanti United.

Azam FC imekuwa na utaratibu mzuri wa kulea wachezaji wake vijana kwa kuwapandisha kwenye timu kubwa, ambao wamekuwa wakifanya vizuri na kuibeba timu, ambapo wengine waliopo katika kikosi cha wakubwa ni makipa Aishi Manula, Metacha Mnata, mabeki Gadiel Michael, Ismail Gambo, kiungo Mudathir Yahya, Abdallah Masoud, Himid Mao, Joseph Mahundi na mshambuliaji Shaaban Idd.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliyeongezewa mkataba wa mwaka mmoja, anaamini ya kuwa wachezaji hao vijana watazidi kukiimarisha kikosi chake kwa kushirikiana na wachezaji wazoefu waliopo kikosini, hadi anafikia uamuzi huo wa kuwapandisha aliwafuatilia katika mechi mbalimbali za timu ya vijana ikiwemo na baadhi ya siku kuwajumuisha katika mazoezi ya timu kubwa.

Aidha kuhusiana na wachezaji waliomaliza mikataba yao, Azam FC imethibitisha rasmi kuachana na winga wake Khamis Mcha ‘Vialli’ na Ame Ally, aliyekuwa kwa mkopo Kagera Sugar, wote mikataba yao ikiwa imemalizika.

Mabadiliko kwenye mfumo wa uongozi

Katika hatua nyingine, Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC imefanya mabadiliko ya mfumo wa kiuongozi ya timu hiyo kwa kukifuta cheo cha Ofisa Mtendaji Mkuu, na sasa cheo cha juu kitakuwa ni Meneja Mkuu, nafasi inayoshikiliwa na Abdul Mohamed.

Kutokana na mabadiliko hayo ya kiutendaji, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, amemaliza mkataba wake na pande zote mbili zimekubaliana kuachana, na sasa majumuku yake yote yatafanywa na Abdul Mohammed, akiwa ndio Meneja Mkuu wa klabu.

Chanzo: Azam FC Official Site

0 comments:

Post a Comment