Sunday, July 24, 2016

BAADA YA KUTUPIWA VIRAGO HAMISI KIIZA AICHANA VIBAYA SIMBA

Hamisi Kiiza ambaye aliingia katika mgogoro na uongozi wa timu yake ya zamani ya Simba SC ameamua kufunguka na kusema kwamba timu hiyo hata isajili nyota wote kamwe haitafanikiwa.

Kiiza aliyeshika nafasi ya pili kwa upachikaji wa magoli ligi kuu Vodacom msimu wa 2015/16 akimaliza kwa kufunga jumla ya magoli 19 amesema Simba hata imsajili Mbwana Samatta anayetumikia klabu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji kamwe haitafika kokote mpaka pale baadhi ya viongozi waondoke katika klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo amedai kwamba kitu kikubwa kinachowasumbua Simba ni uongozi na wala sio wachezaji na hata makocha ambao wamekuwa wakibadilishwa mara kwa mara.

“Sidhani kama kutakuwa na mabadiliko hata kama wakiwasajili wachezaji wote wanaofanya vizuri Tanzania, wamrudishe na Mbwana Samatta, tatizo kubwa lililopo Simba ni baadhi ya viongozi ambao wamekuwa na chuki na wachezaji hasa anaposema ukweli na kudai haki zake,” alisema Kiiza.

Kiiza aliongeza kuwa ameshindwa kumaliza mkataba wake na klabu hiyo kutokana na kutupiwa lawama nyingi katika klabu hiyo ikiwemo ile ya kuambiwa kuwa anaigawa timu, alisema kwamba ingekuwa kweli kuwa anaihujumu timu hiyo basi asingekuwa anafunga magoli pale alipokuwa anapata nafasi ya kufanya hivyo bali ni fitna tu za baadhi ya viongozi klabuni hapo ndio zinazoitafuna klabu hiyo huku akisisitiza kuwa Simba ilikuwa na nafasi ya kufanya vizuri msimu uliopita lakini tatizo kubwa ni huo uongozi.

Hata hivyo Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo Hanspoppe amekanusha tuhuma hizo na kusema kwamba ni benchi la ufundi kwa ujumla wake ndio halikuona haja ya kuendelea kuwa na mchezaji huyo (Kiiza) kutokana na utovu wa nidhamu.
Ungana Na Soka24 Facebook, Bonyeza  HAPA 

0 comments:

Post a Comment