Thursday, June 16, 2016

MATARAJIO YA SIMBA KIKOSI KIPYA MSIMU UJAO

Zacharia Hans Poppe, mwenyekiti wa kamati ya usajili Simba, amesem
a kikosi chao msimu ujao kitakuwa na mabadiliko makubwa kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji.

Simba kwa sasa ipo katika harakati za kuhakikisha wanawanasa wachezaji wazuri watakaoirudisha Simba kwenye makali yao katika ligi msimu ujao. Simba imekuwa ikifanya vibaya takribani miaka mitatu sasa hivyo kuona kila sababu ya kufanya jitihada za makusudi ili kuinusuru klabu hiyo.

Hans Pope amesema lengo lao ni kuhakikisha Simba inakuwa timu tishio kama ilivyokuwa awali na kuchukua taji la ligi kuu Vodacom msimu ujao pamoja na kufanya vizuri katika michuano mingine watakayoshiriki.

"Tunaendelea na kukisuka upya kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wapya katika sehemu ambazo tulikuwa na upungufu, lakini pia tumekubaliana kutafuta kocha mpya mwenye kiwango cha juu kwa ajili ya kuturudisha kwenye mafanikio tuliyokuwa nayo siku za nyuma, mambo yote yanaenda vizuri na ninaamini yatakamilika kwa wakati muafaka" alisema Hans Pope.

Hans Pope alisema tangu kumalizika kwa ligi msimu uliopita wamekuwa wakiendelea na usajili lengo ni kutafuta wachezaji wenye viwango vya kuichezea Simba na kuipa mafanikio.

Aidha Hans Pope alisema kuwa hadi hivi sasa tayari wameshafanya makubaliano na wachezaji watano, na bado wanaendelea kusaka nyota wengine kutoka mataifa ya nje ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wachezaji waliomaliza mikataba yao.

Bonyeza hapa ku-Like Page ya Soka24 Facebook


0 comments:

Post a Comment