Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Van Pluijm ameliomba shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF) kuchukua hatua kali kwa klabu ambazo mashabiki wake wataleta vurugu dhidi ya timu pinzani.
Pluijm ametoa onyo hilo kwa CAF wakati huu michuano ya kombe la shirikisho hatua ya makundi ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni, Yanga wakianza mchezo wao wa kwanza katika hatua hiyo dhidi ya MO Bejaia ya nchini Algeria, mechi itakayochezwa mwishoni mwa wiki hii.
Pluijm amesema kwa miaka mingi kumekuwa na vitendo vya vurugu kwenye mchezo wa soka barani Afrika hasa kwa timu mwenyeji kuifanyia vurugu timu ngeni.
Kocha huyo alitoa mfano wa vurugu ambazo Yanga walifanyiwa kwenye mchezo wa ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ugenini na dhidi ya Sagrada Esperanca ya nchini Angola.
"Vitendo vya vurugu dhidi ya timu ngeni katika soka Afrika sio vya sasa, vipo kwa miaka mingi sana. Sisemi natarajia kukutana navyo katika mchezo dhidi ya MO Bejaia au la, lakini tunatakiwa kujiandaa kisaikolojia kwa lolote" alisema Pluijm.
"CAF wanapaswa kuwa wakali dhidi ya vitendo hivi vya vurugu vinavyofanywa na timu wenyeji kwa wageni wao, wanatakiwa kuchukua hatua kali."
Yanga itacheza mchezo wa kwanza dhidi ya MO Bejaia Juni 19, kisha watarejea nchini kucheza TP Mazembe juni 28.
Bonyeza hapa ku-Like Page ya Soka24 Facebook
0 comments:
Post a Comment