Sunday, June 12, 2016

KIPA YANGA ASAKA KLABU YA KUHAMIA

Baada ya Yanga kufanikiwa kumsajili mlinda mlango kutoka timu ya Tanzania Prisons, Ben Kakolanya, Mlinda mlango wa siku nyingi wa klabu hiyo, Benedictor Tinoco amesema ni wakati wake kuangalia sehemu gani atacheza msimu ujao.

Usajili wa Kakolanya unawafanya Yanga kuwa na magolikipa wanne ambao ni Ally Mustafa, Deogratius Munish, Kakolanya pamoja na Benedictor Tinoco, Tinoco tangu asajiliwe msimu uuliopita akitokea Kagera Sugar hajapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Mkataba wake na klabu ya Yanga haujaisha lakini ujio wa kipa mpya kikosini hapo unaonyesha wazi kuwa anahitaji kwenda kujaribu sehemu nyingine ili kulinda kiwango chake kisishuke.

"Siwezi kukaa Yanga milele, nahitaji kuangalia mbele na kutafuta timu ambayo itanisaidia kulinda kiwango changu na kutimiza ndoto zangu" alisema Tinoco.

Tinoco anatamani kupata timu ambayo ataweza kucheza kwani yeye mwenyewe anaamini uwezo anao mkubwa isipokuwa hakuwahi kupata nafasi ya kuonyesha kipaji chake Yanga.

Ushindani uliopo katika klabu ya Yanga umefanya idadi ya wachezaji wanaoomba kuondoka klabuni hapo kufikia watatu sasa, baada ya Paul Nonga kuandika barua kwa uongozi wa timu hiyo akiomba wamuuze, Malimi Busungu nae ametajwa kuomba kwenda kujiunga Stand United ili kulinda kiwango chake pamoja na Tinoco ambaye anahofia nafasi yake Jangwani kwa sasa.

0 comments:

Post a Comment