Wednesday, May 25, 2016

YANGA IJIPANGE VIZURI ITAKAPOKUTANA NA TIMU HIZI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

Draw ya kombe la shirikisho hatua ya makundi imeshafanyika na tayari imeshafahamika nani atakutana na nani katika hatua hiyo.



Bingwa wa ligi kuu Tanzania bara 2015/16 Young Afrikans imepangwa katika kundi A ambalo lina timu za TP Mazembe ya DR Congo, MO Bejaia ya Algeria na Medeama kutoka Nchini Ghana.

Yanga imetinga hatua hii baada ya kuiondosha Sagrada Esperanca ya nchini Angola baada ya kushinda goli 2 - 0 katika mchezo uliochezwa hapa Tanzania na kufungwa goli moja kule nchini Angola hivyo Yanga kusonga mbele kwa jumla ya magoli ambayo ilikuwa 2 - 1.

Wawakilishi hawa pekee wa Tanzania sasa wametinga hatua ya robo fainali na tayari wameshajua timu watakazokutana nazo. Katika hatua hii hakuna timu ya kuidharau, Timu zote ni nzuri na ndio maana zimefika hapa. Kihistoria Yanga ilishawahi kutinga hatua hii ya 8 bora mwaka 1998  wakati huo timu ikiwa chini ya Tito Mwavalunda kama kocha mkuu akishirikiana na Felix Minziro.

Watanzania tunajivunia hatua hii waliyofikia Yanga na tunapenda tuendelee kuiona timu yetu ikipeperusha vyema bendera ya Taifa letu kwani ni kitu ambacho kitaleta faida kubwa nchini hasa katika nyanja hii ya Mpira wa miguu.

Yanga inatakiwa kuwa makini sana na kujipanga vizuri zaidi hasa itakapocheza na timu zifuatavyo, iwe nyumbani au Ugenini;

MO Bejaia

Hawa ni Waarabu wa kutoka Algeria, timu hii ilianzishwa mwaka 1954 kiumri Yanga ni kubwa ukilinganisha na timu hii, kwa miaka ya hivi karibuni kasi ya ukuaji wa mpira katika nchi ya Algeria imekuwa kubwa sana na Timu ya Taifa ya Algeria ndo inashika namba moja kwa sasa katika bara la Afrika. MO Bejaia haina jina kubwa sana katika michuano ya CAF, kwa maana Champions League na Confederation Cup, lakini ni timu tishio sana kwa siku za hivi karibuni, MO Bejaia ndo imewaondoa Esperanca ambao waliwahi kucheza na Azam FC na Azam kuondolewa. Licha ya kuiondosha Esperanca ya Tunisia bila shaka tunajua wazi fitina za Waarabu katika mpira wa miguu, wanamambo mengi sana ambayo sio ya kiungwana, wanayafanya ili tu kuiharibu timu pinzani kisaikolojia na kimazingira pia ilimradi tu wao wapate ushindi. Hili Yanga wanapaswa kulitambua mapema na kulifanyia kazi na sio kusubiri kutolewa na kuanza kulalamika, tumeona waliyoyafanya Waangola katika mchezo wa marudiano uliofanyika Angola dhidi ya Yanga, walifanya figisu nyingi sana lakini hili sisi hatuliwezi, hatusemi wawafanyie vitu vibaya wakifika hapa, HAPANA ila kwa muda mrefu sasa tumeona vitimbwi tunavyofanyiwa na wenzetu hasa tukienda ugenini, Azam Fc walifanyiwa uhuni na El Merrikh Sudan wakapandishwa kwenye gari bovu kabisa na Azam waliharibiwa kabisa Kisaikolojia na hatimaye walifungwa na kutolewa mashindanoni, ipo mifano mingi na bila shaka uongozi wa Yanga watakuwa wanalijua hili.

TP Mazembe

Kila Mpenda Soka Afrika anatambua uwepo wa Mazembe katika ulimwengu wa soka, ni timu tajiri na ni Bingwa mara tano wa klabu Bingwa Afrika wakishinda miaka ya 1967, 1968, 2009, 2010 na 2015. Wamewahi kucheza fainali ya klabu bingwa duniani dhidi ya Inter Milan. Kiufupi ni timu yenye uzoefu mkubwa katika michuano ya CAF. Wapo wanaosema kuondoka kwa Mbwana Samatta kumepunguza makali ya TP Mazembe ni kweli lakini hiyo haitoshi kuwa sababu ya Yanga kuidharau Mazembe. Ni moja ya Timu Bora Afrika ikijumuisha wachezaji kutoka katika mataifa mbalimbali. Yanga wanatakiwa kuhakikisha wanaibuka na pointi tatu katika mechi ya nyumbani dhidi ya Mazembe ili kujihakikishia nafasi nzuri katika kundi hilo.Mazembe Wametolewa katika michuano ya klabu bingwa Afrika na ni wazi kuwa watahitaji kurudisha heshima yao kwa kuhakikisha wanaingia katika hatua ya nusu fainali na hata kutwaa ubingwa hivyo haitakuwa rahisi kwa Yanga kupata pointi kwa Wakongo hawa hasa katika mechi itakayopigwa Lubumbashi.


Wanasoka tunaamini katika mpira kila kitu kinawezekana, imani hiyo pia timu nzima ya Yanga wanatakiwa kuwa nayo na kuiishi, inawezekana kwa Yanga kutinga hatua ya Nusu fainali na hata kuchukua taji hilo cha msingi ni kujipanga vizuri na kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi zao zote za nyumbani.



Medeama sio timu ya kubeza pia japo kocha Hans anaweza kuwa na mbinu sahihi za kuzitumia pale watakapokutana ikizingatiwa kuwa Hans amewahi kuifundisha Medeama hivyo kwa kiasi fulani atakuwa anawajua vizuri.

KILA LA KHERI YOUNG AFRICANS 

0 comments:

Post a Comment