Saturday, May 14, 2016

REAL MADRID YAPOTEZA MASHABIKI 16 KATIKA SHAMBULIZI LA KIGAIDI

Kulia ni mashabiki waliokufa katika shambulizi hilo

Mabingwa mara 10 wa kombe la UEFA Champions league Real Madrid watafunga vitambaa vyeusi katika mikono yao kuomboleza vifo vya mashaki wao 16 waliopoteza maisha katika shambulio la kigaidi huko nchini Iraq.

Wakati Real Madrid wakifanya maandalizi ya mwisho kuelekea katika mchezo wao muhimu zaidi katika ligi dhidi ya Deportivo, mchezo ambao huenda ukaamua mshindi wa kombe la La Liga msimu huu, klabu hiyo imestushwa na taarifa za vifo vya mashabiki wake 16 vilivyotokea nchini Iraq.

Mashabiki hao 16 waliokuwa wakijulikana kwa jina la Merengue, kikundi kilichokuwa kinaisapoti Real Madrid, wamepoteza maisha katika shambulizi la kigaidi usiku wa  Alhamisi huku 20 wengine wakijeruhiwa vibaya hali inayoonyesha huenda nao wakapoteza maisha muda wowote.

Ripoti inasema kwamba mashabiki hao walikusanyika katika Café moja inayojulikana kwa jina la Al Furat katika jiji la Balad kaskazini mwa mji mkuu wa Baghdad, ndipo mtu mmoja aliyekuwa amebeba silaha anayehusishwa na kundi la kigaidi la ISIS alipoingia katika Café hiyo na kuanza kumimina risasi kwa waliokawemo ndani humo.
Picha ya eneo lilipotokea tukio hilo

Real Madrid walituma salamu zao za rambirambi kwa familia zilizopatwa na  misiba hiyo wakiandika katika tovuti yao kuwa “Klabu ya Real Madrid inalaani vikali shambulizi hilo baya la kigaidi nchini Iraq lililofupisha maisha ya watu 16 wanachama wa kikundi kilichokuwa kinaisapoti Real Madrid, sambamba na wengine 20 waliojeruhiwa”

Wapinzani wao klabu ya Barcelona nao wameonyesha masikitiko yao juu ya tukio hilo, wakitoa pole pia kwa familia zilizokutwa na janga hilo.

Barcelona wameandika maneno haya katika akaunti yao ya Twitter “FC Barcelona inatoa pole kwa wahanga wa shambulizi lililotokea Iraq lililowahusisha wanachama wa kikundi kinachoisapoti Real Madrid”

Mungu azilaze roho za marehemu hao mahala pema peponi na awaponye wote waliojeruhiwa ili warudi katika shughuli zao za kila siku. Amen

0 comments:

Post a Comment