Zeben Hernandez Kocha Mpya Azam FC |
KOCHA Mkuu mtarajiwa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa malengo yake makubwa ni kuifanya timu hiyo kuwa timu kubwa barani Afrika msimu ujao.
Kocha huyo raia wa Hispania aliyekuwa akiinoa Club Deportivo Santa Ursula ya Ligi Daraja la Tatu nchini humo, ametua nchini juzi pamoja na Kocha wa Viungo Jonas Garcia kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa timu hiyo kabla ya kusaini mkataba wa kuinoa Azam FC msimu ujao.
Makocha hao wametua kufuatia Kocha Mkuu wa sasa wa Azam FC, Stewart Hall, kutangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu kufuatia kutoridhishwa na matokeo ya hivi karibuni ya timu hiyo.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz leo asubuhi mara baada ya kuwasili mkoani Tanga kushuhudia mchezo wa timu hiyo dhidi ya African Sports jioni ya leo, Hernandez amewaambia mashabiki wa Azam FC kuwa watarajie ubora wa timu msimu ujao utakaoifanya kuwa timu bora Afrika.
“Ninafuraha kubwa, Azam itakuwa timu bora msimu ujao, tutafanya kazi kwa bidii kila mara na kuifanya Azam kuwa timu kubwa Afrika,” alisema.
Aifurahia Tanzania
Hernandez hakusita kuelezea furaha yake kutokana na watu aliokutana nao Tanzania, ambapo amesema kuwa: “Ninafuraha kubwa, watu wa hapa ni wazuri na waliojipanga, na mpira wa hapa una vipaji vingi, wachezaji wengi kuwa na vipaji ni jambo muhimu kwa mpira wa Tanzania, Tanzania kama nchi ni sehemu nzuri sana na ninafuraha sana kwa hilo.”
Ujio wao ndani ya Azam FC
“Malengo yetu ni kuifanya Azam kuwa na mfumo mpya wa soka la kisasa kuanzia utambulisho kama timu, mbinu zetu za kufanya kazi na pia katika mechi…Kwangu mimi na mwenzangu kufanya kazi Afrika ni uzoefu mzuri na tunafuraha sana,” alisema.
Kwa upande wake Jonas Garcia aliyeambatana naye alionyesha furaha kubwa kuja Azam FC huku akisema kuwa watafanya kazi kwa bidii sana kwa ajili ya kuipa ubora timu hiyo.
C.E.O afafanua ujio wao
Akizungumzia ujio wa makocha hao, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, amesema kuwa mara baada ya kuwasili juzi tayari wameanza nao mazungumzo jana kwa ajili ya kukinoa kikosi hicho msimu ujao.
“Tumewapokea juzi Dar es Salaam tunamshukuru Mungu, jana tulikuwa nao na tumeanza mazungumzo, leo wako hapa Tanga kuangalia mchezo (African Sports vs Azam FC) na watafanya tathimini yao, kwa hiyo mazungumzo bado yanaendelea na katika hali ya kawaida tukifanikiwa kwa maana yake watakuwa wanachukua timu yetu ya Azam kwa msimu unaokuja, jambo jema kwetu ni kwamba makocha hao bado ni vijana na wanadhamira ya kupata mafanikio, hivyo hiko ni kitu ambacho tunajivunia.
“Lakini bado tunasema kwamba bado tunazungumza nao hatujafika nao muafaka mpaka mwisho, lakini tunachopenda kusema ni kwamba tunawaomba mashabiki wetu wawe watulivu timu ipo na kocha bado yupo (Stewart Hall) na anamalizia muda wake na kuhakikisha ya kuwa kila kitu kinakwenda sawasawa kabla ya msimu haujaisha,” alisema.
Bosi huyo aliyebobea kwenye mambo ya uongozi wa soka na kutambulika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Duniani (FIFA), alimalizia kwa kusema kuwa wanatarajia kufanya mkutano na waandishi wa habari kesho Jumatatu mara baada ya kumalizia mazungumzo ya mwisho na makocha hao, ambapo ataweka wazi kila kitu kuhusu muundo wa benchi la ufundi msimu ujao.
SOURCE: AZAM FC OFFICIAL SITE
0 comments:
Post a Comment