Kocha anayechukua mikoba ya Pep Guardiola katika klabu ya Bayern Munich Carlo Ancelotti amesema ipo siku Guardiola atatimuliwa kama mbwa katika maisha yake ya ukocha.
Ancelotti amemuonya Pep kwamba katika maisha yake ya ukocha atakuja kutimuliwa siku moja akisisitiza kuwa ni kitu ambacho hakuna kocha yoyote duniani anaweza akakikwepa.
Ancelotti anayeonekana kuwa miongoni mwa makocha bora duniani kwa sasa ameshinda taji la UEFA Champions league akiwa na AC Milan na Real Madrid. Carlo pia ameshinda kombe la Serie A, English Premier League, FA Cup na Ligue 1 lakini hata hivyo ameshawahi kutimuliwa mara kadhaa katika maisha yake ya ukocha.
Alitimuliwa na Chelsea licha ya kushinda ligi kuu mara 2 sawasawa na kilichomtokea akiwa Real Madrid akiipa Madrid ubingwa wa 10 wa UEFA Champions League.
Ancelotti ameyasema hayo kufuatia rekodi za Guardiola, Pep ni miongoni mwa mameneja wachache waliopata mafanikio makubwa akiwa na klabu zote za Barcelona na Bayern Munich na katika klabu hizo zote mbili Guardiola aliondoka kwa kupenda kwake na sio kutimuliwa.
Lakini akiwa anajiandaa kukabiliana na kibarua kizito zaidi cha kuinoa Manchester City, Ancelotti amemuonya Guardiola kwamba itakuja itokee Guardiola nae kuwa katika orodha ya makocha waliowahi kuonja machungu ya kutimuliwa na klabu kubwa.
Akiwa katika mahojiano na The Times Ancelotti alisema “ Nikiwa Chelsea nilishinda mara 2 ligi kuu, ila niliishia kutimuliwa, Madrid nako nimewapa taji la 10 UEFA Champions bado wakanitimua”
“Kocha ambaye hajawahi kutimuliwa ni Guardiola pekee, Sir Alex Ferguson alishatimuliwa, Marcelo Lipi kafukuzwa, Fabio Capello kafukuzwa, Jose Mourinho kafukuzwa, Rafa Benitez kafukuzwa”
“Ni Guardiola tu ndiye ambae hajawahi kufukuzwa, lakini bado ni mdogo na ana muda mwingi wa kufanya kazi, siku moja atakuja katika klabu yetu, klabu ya makocha waliowahi kutimuliwa”
0 comments:
Post a Comment