Saturday, August 13, 2016

MATUMAINI PEKEE YALIYOBAKI KWA YANGA

Kikosi cha Yanga leo kinatarajia kuishukia Mo Bejaia ya Algeria kama mwewe kwenye mchezo wa marudiano wa Kundi A, Kombe la Shirikisho utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa ni vibonde katika kundi lao hilo, kwa kuwa haijaambulia ushindi hata wa goli moja baada ya kunyukwa 1-0 na Mo Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Medeama kwenye Uwanja wa Taifa na baadaye kwenda kufungwa 3-1 na timu hiyo nchini Ghana katika mchezo wa marudiano.

Yanga Leo inahitaji ushindi kwa hali yoyote ili wafufue matuamaini ya kuwania kucheza hatua ya Nusu fainali katika michuano hiyo ya kombe la shirikisho Barani Afrika (CAF CC), lakini matuamaini hayo yatatimia endapo tu Mchezo kati ya TP Mazembe na Medeama utakaopigwa nchini Ghana, Mazembe ataifunga Medeama na kuwafanya Medeama na Mo Bejaia kubaki na pointi zao 5 katika msimamo wa kundi A, ambapo Yanga atafikisha Pointi 4.

Na katika michezo ya mwisho ya kundi A, Yanga wanatakiwa kuifunga TP Mazembe kwao nchini Congo wakati huo wakiomba mechi kati ya MO Bejaia dhidi ya Medeama utakaopigwa nchini Algeria uishe kwa suluhu au sare yoyote, hapo Yanga itakuwa imefikisha pointi 7, wakati MO Bejaia na Medema watakuwa na pointi 6 kila mmoja, hivyo Yanga kushika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi A kwa kufikisha pointi 7 huku Mazembe akiwa na pointi 13 katika nafasi ya kwanza.

Akizungumzia mchezo wa leo kocha mkuu wa klabu ya Young Africans, Hans Van Pluijm amesema hautakuwa mchezo rahisi kwao licha ya kuwa wanatakiwa kupambana kadri wawezavyo ili kuhakikisha wanapata pointi tatu

"Mechi itakuwa ngumu, lakini katika soka hauwezi kukata tamaa mapema tena kwa rahisi namna hiyo. Kama tutashinda, basi tuna nafasi bado,” alisema Pluijm.

Mechi itaanza majira ya Saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki
Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook, Bonyeza  HAPA 





0 comments:

Post a Comment