Thursday, June 23, 2016

MATUMAINI YA CANNAVARO KUELEKEA MCHEZO NA MAZEMBE

Nahodha wa klabu ya Yanga, Nadir Haroub Cannavaro anaamini kuwa kikosi chao kitatinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho Barani (CAF CC).

Yanga ambayo imepoteza mchezo wake wa kwanza kwa kukubali kipigo cha goli moja kwa bila kutoka kwa MO Bejaia ya nchini Algeria, itashuka dimbani tena kucheza na mabingwa wa Afrika timu ya TP Mazembe ya Congo DRC.

Cannavaro alikosa mchezo wa kwanza dhidi ya MO Bejaia kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wa kufuzu hatua ya makundi dhidi ya Sagrada Esperanca ya nchini Angola, Nahodha huyo amefurahishwa na kiwango walichokionyesha Yanga katika mchezo na Mo Bejaia licha ya kufungwa goli hilo moja.

"Naweza kusema tulikosa bahati katika mchezo ule kwa sababu timu ilicheza vizuri na tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini tulishindwa kuzitumia na hicho ndicho kinanipa imani kama Yanga inaweza kucheza nusu fainali hata fainali mwaka huu" alisema Cannavaro.

Aidha Nadir alisema mipango yao ni kufanya mazoezi yakutosha ili kuikabili TP Mazembe, mchezo utakaochezwa Juni 28.

"Kocha Hans Pluijm na wenzake wa benchi la ufundi watakuwa wameona udhaifu wetu katika mchezo uliopita, hivyo watafanyia kazi kwenye mazoezi yetu kuelekea mchezo na Mazembe" aliongeza Nahodha huyo.

Yanga imeomba kwa shirikisho la soka Tanzania TFF kuiandikia barua CAF kuomba mechi yao na Mazembe ichezwe Juni 29 saa moja na nusu usiku badala ya Juni 28 saa 10:00 jioni.

Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook Hapa

0 comments:

Post a Comment