Sunday, April 24, 2016

MATCH PREVIEW: Mwadui VS Azam FC


LEO ndio leo ndani ya Uwanja wa Mwadui, mjini Shinyanga, ambapo utashuhudiwa mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC kuvaana na wenyeji wao Mwadui FC saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na historia za timu zote mbili kila zinapokutana, ambapo tayari kila upande umejinasibu kuondoka na ushindi na kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.

Azam FC inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo kutokana na mipango waliyojiwekea ya kutwaa taji hilo na vilevile kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kushinda mechi sita walizobakiza hadi sasa.

Nusu fainali nyingine itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga leo, itawakutanisha wenyeji Coastal Union walioitoa Simba katika raundi iliyopita wataikaribisha Yanga iliyoitoa mashindanoni Ndanda ya Mtwara, mchezo mwingine unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake hasa ikizingatiwa Wanajangwani hao walifungwa bao 1-0 walipokutana na Wagosi wa Kaya hao ndani ya dimba hilo kwenye mechi ya ligi.

Tunataka kuingia fainali

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa mchezo huo ni muhimu sana kwao kwani ikizingatiwa wanataka kuingia fainali ya michuano hiyo.

“Kiukweli mchezo huo ni muhimu sana kwetu, tunataka kuingia fainali, jambo la kwanza tunataka kurudisha ari za wachezaji vizuri mara baada ya matokeo mabaya tuliyopata Tunisia, tunatakiwa kuondoa hilo akilini mwa wachezaji na kuwafikirisha zaidi umuhimu wa mchezo huo, huwezi kubadilisha jambo lililotokea bali unatakiwa kuangalia mbele ili kufanya vizuri.

“Kwa sasa tuna wachezaji sita wanaoumwa kidogo kutokana na uchovu, tutajua hali zao zinaendeleaje kikao cha mwisho kesho (leo) kabla mchezo huo, hatuna majeruhi wapya, tunashukuru Migi na Himid wanarejea kikosini ambao wako vizuri kiafya, Vialli (Khamis Mcha) naye yupo vizuri,” alisema.

Hata hivyo kwenye mazoezi ya mwisho ya Azam FC yaliyofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza jana jioni, wachezaji wa timu hiyo walionekana kucheza kwa bidii hasa baada ya kutambua ya kuwa mchezo huo una umuhimu mkubwa sana kwao kama wataibuka na ushindi.  

Hall alisema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu sana kutokana na aina ya timu wanayoenda kukutana akikumbushia namna walivyoonyeshwa upinzani mkali katika mechi mbili zilizopita walizokutana nao kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

“Utakuwa ni mchezo mgumu kwa sababu wachezaji wao wanatujua vizuri na timu yao imeundwa na wachezaji wengi wazoefu, tunajua namna ya kukabiliana nao, tulivyokutana nao mara mbili huko nyuma hatukuwa vizuri, mchezo wa kwanza tulioshinda 1-0 tulicheza tukiwa pungufu kwa takribani dakika 45 baada ya Aggrey Morris kuonyeshwa kadi nyekundu, pia wa pili tuliokutana nao na kushinda tena 1-0 Azam Complex, tulicheza tukiwa na uchovu mara baada ya kurejea kutoka Zambia,” alisema.

Rekodi zao

Huo utakuwa ni mchezo wa tatu wa mashindano kwa timu hizo kukutana kwani hapo awali zimekutana mara mbili kwenye ligi tokea Mwadui ilipopanda daraja msimu huu.

Zimefikaje hatua hiyo

Mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), wamefika hatua hiyo baada ya kuzitoa timu za African Lyon, Panone na Tanzania Prisons huku Mwadui nayo ikizitupa nje Stand United, Rhino Rangers na Geita Gold.

Azam FC ilianza kwa kuichapa African Lyon mabao 4-0 katika hatua ya 32 bora, kabla ya kuidungua Panone 2-1 (16 bora) na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuitandika Tanzania Prisons 3-1.

Mwadui inayonolewa na moja ya makocha wenye mbembwe nyingi na mzoefu, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, yenyewe ilianza kwa ushindi mwembamba kwa kuwachapa ndugu zao Stand United 1-0, katika hatua ya 16 bora ikaicharaza Rhino Rangers 3-1 na kutinga nusu fainali kwa kuichapa Geita Gold 3-0, zote hizo mbili zikishiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita.

Hadi inatinga hatua ya nusu fainali, Azam FC imefunga jumla ya mabao tisa katika mechi tatu na kufungwa mawili pekee huku Mwadui ikitupia saba na kufungwa moja tu walipokipiga na Rhino Rangers ya mkoani Tabora.

Bingwa wa FA Cup

Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kurudisha michuano hiyo tena msimu huu, sasa bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani (CC) badala ya mshindi wa pili wa ligi iliyokuwa ikitumika kwa takribani miaka 14 iliyopita mashindano hayo yalipokufa.

Hivyo kama Azam FC ikitwaa ubingwa huo itakuwa imejihakikishia nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya pili kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.

Kama ikitokea Azam FC ikitwaa ubingwa huo pamoja na taji la ligi basi hiyo itamaanisha ya kuwa itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani na aiyeshika nafasi ya pili kwenye FA Cup atashiriki Kombe la Shirikisho.

Usikose Kufuatilia Mechi Hiyo Kwa Kila Litakalojiri huko Shinyanga kupitia soka24.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment