Friday, February 24, 2017

Zijue Rekodi Za Azam FC Vs Mtibwa Sugar

KESHO ndio kesho ndani ya Uwanja wa Azam Complex, utashuhudiwa mchezo mkali wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baina ya wenyeji Azam FC na Mtibwa Sugar, utakaoanza saa 10.30 jioni

Mabingwa hao wanaoshikilia mataji matatu; la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi, hivi sasa wapo kwenye maandalizi makali kujiandaa na mchezo huo, ambao wanauchukulia kwa uzito mkubwa.

Hii ni mara ya kwanza timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, iliyorejeshwa msimu uliopita baada ya kutofanyika kwa miaka kadhaa iliyopita.

Kuelekea mtanange huo, zifuatazo ni baadhi ya takwimu kwenye mechi rasmi walizowahi kukutana katika mashindano mbalimbali, ambazo zinaonyesha kuwa wamekutana mara 19, zikiwa ni mechi 17 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na mbili za Kombe la Mapinduzi.

Katika mechi 17 za ligi walizokutana tokea Azam FC ipande daraja mwaka 2008, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex ndio wanarekodi bora wakiwa wameshinda robo tatu ya mechi hizo yaani mara tisa, Mtibwa Sugar ikishinda mara mbili tu na michezo sita wakienda sare.

Kati ya mechi hizo nane ambazo ilishindwa kuibuka na ushindi, ni mechi tano tu ambazo Azam FC ilicheza nyumbani, ikifungwa mmoja wakati huo ikitumia Uwanja wa Uhuru kwa mechi za nyumbani na kutoka sare mara nne.

Katika rekodi hiyo ya ushindi, Azam FC imeonekana kuwa na uwiano mzuri wa kushinda ugenini, ikishinda michezo mara tano huku ikiwa imeibuka kidedea mara nne nyumbani.

Ushindi unaokumbukwa ni ule walioibugiza mabao 5-2 Mtibwa Sugar msimu wa 2014/15 wakati ikifundishwa na Mcameroon, Joseph Omog, anayeifundisha Simba hivi sasa, huku katika rekodi hiyo ikionyesha kuwa wamewahi kuwapiga Wakatamiwa hao 4-0 msimu wa 2010/2011.

Katika mechi hizo 17, jumla ya mabao 38 yamefungwa ukiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.2 katika kila mchezo, Azam FC ikiwa inaongoza ikiwa imetupia 26 huku Mtibwa Sugar ikiuona wavu wa matajiri hao mara 12 tu.

Mara mbili walizokutana kwenye Kombe la Mapinduzi, mwaka juzi zilitoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye robo fainali na Azam FC kutolewa kwa mikwaju ya penalty 7-6 huku mwaka jana zikitoka sare kama hiyo katika mchezo wa hatua ya makundi.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana, ilikuwa ni Desemba mwaka jana kwenye mchezo wa kirafiki ulioisha kwa sare ya mabao 2-2, mabao ya Azam FC yakitupiwa wavuni na Enock Atta Agyei kwa mkwaju wa penalti na Yahaya Mohammed.

Pia msimu huu katika mzunguko wa kwanza wa ligi zilikutana ndani ya Azam Complex na kutoka sare ya baoa 1-1, bao la Azam FC likifungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’ huku Mtibwa iliyotangulia kupata bao ikijipatia kupitia kwa mshambuliaji, Rashid Mandawa, aliyewahi kuchezea timu ya vijana ya Azam FC.

Jionee mechi zote za mashindano;

VPL Games (17)

19/10/16   Azam FC 1 – 1  Mtibwa Sugar (Sare)

13/04/16   Mtibwa Sugar  0 – 1 Azam FC (Azam FC Ushindi)    

30/12/15  Azam FC  1 – 0  Mtibwa Sugar (Azam FC Ushindi)      

11/04/15  Mtibwa Sugar 1 – 1  Azam FC (Sare)        

11/02/15  Azam FC  5 – 2  Mtibwa Sugar (Azam FC Ushindi)      

25/01/14  Azam FC  1 – 0  Mtibwa Sugar (Azam FC Ushindi)        

24/08/13  Mtibwa Sugar  1 – 1  Azam FC (Sare)        

10/02/13  Mtibwa Sugar  1 – 4  Azam FC (Azam FC Ushindi)                          

22/09/12  Azam FC  1 – 0  Mtibwa Sugar (Azam FC Ushindi)        

04/05/12  Azam FC  1 – 2  Mtibwa Sugar (Mtibwa Ushindi)        

25/10/11  Mtibwa Sugar  1 – 0  Azam FC (Mtibwa Ushindi)

13/03/11  Azam FC  2 – 2  Mtibwa Sugar (Sare)        

20/10/10  Mtibwa Sugar  0 – 4  Azam FC (Azam FC Ushindi)        

25/02/10  Azam FC  0 – 0  Mtibwa Sugar (Sare)        

10/10/09  Mtibwa Sugar 0 – 1  Azam FC (Azam FC Ushindi)      

15/03/09  Azam FC  1 – 1  Mtibwa Sugar (Sare)      

02/11/08  Mtibwa Sugar  0 – 1  Azam FC (Azam FC Ushindi)

Kombe la Mapinduzi (2)

03/01/16 Azam FC 1 – 1  Mtibwa Sugar (Sare)

08/01/15 Mtibwa Sugar 1 – 1 Azam FC (Mtibwa ikashinda kwa penalti 7-6)

Chanzo: AzamFC Official Site

0 comments:

Post a Comment