Friday, February 24, 2017

Simba Vs Yanga:Lwandamina, Omog Watambiana

Februari 25, ni siku inayosubiriwa kwa hamu kubwa kwa wapenzi wa soka nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambapo watani wa jadi, klabu za Simba na Yanga zinatarajia kumenyana katika uwanja wa taifa katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara maarufu kama Vodacom Premier League (VPL) Msimu wa 2016/17.


Ukubwa wa mechi hiyo si tu unatokana na utani uliopo baina ya timu hizo bali pia, hali halisi ya msimamo wa ligi hivi sasa, ambapo tofauti ya pointi kati ya klabu hizo ni pointi moja tu, Simba wakiwa kileleni baada ya kujikusanyia alama 51 katika michezo 22 waliyocheza, huku mahasimu wao Yanga wakishika nafasi ya pili kwa kujikusanyia jumla ya alama 49 katika michezo 21 waliyocheza.

Kuelekea mchezo huo kumekuwa na majigambo mengi kutoka kwa mashabiki wa kila timu wakiamini timu yao ndio itaibuka na ushindi katika mchezo huo, na kwa jinsi hali ilivyo na ushindani mkubwa uliopo katika ligi msimu huu wa 2016/17, mechi hiyo inasemwa kuwa ndio inayoweza kutoa mwangaza wa nani anaweza kuibuka bingwa wa ligi kuu kwa msimu huu, hali ambayo inaongeza ugumu wa pambano hilo.

Makocha wa timu zote mbili wametoa kauli zao kuelekea mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi, Feb. 25 katika uwanja wa Taifa jijini Dar.

“Ukweli kwamba ubingwa wetu msimu huu upo kwenye mchezo dhidi ya Yanga, na tumejipanga kuhakikisha tunashinda hatupo tayari kuona tuna tunafungwa au kutoka sare kwasababu huo ndiyo mchezo pekee mgumu kwetu na endapo tutawafunga itakuwa tumewaacha idadi kubwa ya pointi,”amekaririwa Omog.

Kwa upande wake nae kocha mkuu wa Yanga amesema kitu kikubwa kwao na cha msingi zaidi ni kuiondoa Simba katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.

“Kitu cha msingi kwetu kabla ya kuwaza ubingwa ni kuiondoa Simba, kwenye nafasi ya kwanza na hilo nina uhakika tunaweza kulitimiza katika mechi tatu zijazo, kutokana na ari tuliyokuwa nayo hivisasa na idadi ndogo ya pointi tuliyokuwa nayo kati yetu na wao,” alikaririwa Lwandamina.

0 comments:

Post a Comment