Sunday, January 29, 2017

Sadio Mane Aiponza Senegal Robo Fainali AFCON

Robo fainali ya pili ya AFCON iliyochezwa jana majira ya saa 4:00 usiku kati ya Senegal dhidi ya Cameroon ilikuwa ni ya aina yake.

Katika mchezo huo, ilishuhudiwa miamba hiyo ikimaliza dakika zote 120 bila kufungana, hali iliyopelekea kupigwa kwa mikwaju ya penati.

Katika mikwaju hiyo ya penati Senegal waliondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa kwa penati 5-4, huku Sadio Mane akikosa penati pekee kwa upande wa Senegal.

Senegal ndio waliokuwa wakianza kupiga mikwaju hiyo, walifanikiwa kutupia nyavuni mikwaju yote minne ya awali kabla penati iliyopigwa na mshambuliaji wa kutegemewa wa Liverpool kuokolewa na mlinda mlango kinda wa Cameroon Fabrice Ondoa (21).
Fabrice Ondoa akishangilia baada ya Aboubakar Kukwamisha Nyavuni Mkwaju Uliowapeleka Cameroon hatua ya Nusu Fainali AFCON

Ondoa ndiye alikuwa  shujaa wa mchezo huo na alichaguliwa kuwa "Man Of The Match".
Kuondolewa kwa Senegal katika michuano hiyo kumeleta simanzi kubwa kwa wananchi wa Senegal lakini imekuwa ni furaha kubwa kwa mashabiki wa Liverpoool ambao kwa sasa nyota wao atarudi kikosini wakati huu Liverpool inaposuasua.

Tayari Burkina Faso na Cameroon wamejihakikishia nafasi katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo huku ikisubiriwa michezo ya robo fainali itakayopigwa leo kati ya Congo DR dhidi ya Ghana mechi itakayopigwa mnamo saa 1:00 Jioni kwa majira ya Afrika Mashariki huku Misri dhidi ya Morocco wakihitimisha michezo ya hatua hiyo ya robo fainali hapo saa 4:00 usiku leo Jumapili januari 29.

0 comments:

Post a Comment