Tuesday, January 31, 2017

Omog:"Mashabiki Simba Wakubaliane Na Matokeo"

Kocha Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi Simba, amewataka wapenzi na mashabiki wa Simba kuwa watulivu na kukubaliana na matokeo.

Simba iliyokuwa inaongoza katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara, imeshushwa katika nafasi ya pili baada ya kukubali kipigo cha goli moja kwa bila kutoka kwa Azam FC huku mahasimu wao Yanga wakichomoza na ushindi katika mchezo wao dhidi ya Mwadui FC na kuwafanya kupaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo huku wakiwazidi wapinzani wao kwa alama moja tu.

Omog amesema mashabiki wanatakiwa kuwa watulivu kwani bado wanayo nafasi ya kurekebisha makosa na kufanya vizuri katika mechi zijazo na hatimaye kutwaa ubingwa.

“Hakuna anayependa kufungwa au kutolewa kwenye nafasi nzuri , lakini mashabiki wanapaswa kujua Simba siyo lazima kila siku ishinde ingawa malengo yetu ni ushindi, hivyo inapotokea tumepoteza mchezo kama ilivyotokea Jumamosi wanatakiwa tukubaliane na matokeo alafu tujipange kwa mechi nyingine,”amesema Omog

Kocha huyo amekiri kuwa amekuwa na wakati mgumu sana kufuatia kipigo hicho walichopokea kutoka kwa Azam na kusema kwamba yeye pamoja na wachezaji wameumizwa sana na matokeo ya mchezo huo lakini pia akikir kuwa mpira ni mchezo wa makosa, anakubali walifanya makosa yaliyopelekea wao kupoteza katika mchezo huo.

Kitendo cha Mkameruni huyo kutowaanzisha wachezaji Shiza Kichuya na Ibrahimu Ajib kiliwakera sana mashabiki na kutaka kufikia hatua ya kumpiga kocha huyo kwa kile walichosema ni upangaji mbovu wa kikosi.

0 comments:

Post a Comment