Tuesday, October 11, 2016

MO,MANJI KIKAANGONI OCTOBA 20,2016

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa kongamano maalumu Oktoba 20 mwaka huu, kuzungumzia mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zipo mbioni kuingia.

Simba na Yanga, zipo katika mchakato wa kubadilisha mfumo wao wa kiuendeshaji, ambapo Simba inataka kuingia utaratibu wa hisa huku Yanga ikitaka kukodishwa.

Taarifa ya Taswa kwenda kwa vyombo habari jana ilisema inaamini yapo mambo ambayo wanachama, mashabiki na hata wadau wa mpira wa miguu na wanamichezo kwa ujumla wanapaswa kufahamu kwa undani zaidi kuhusu mifumo hiyo miwili ili kuwe na uelewa mpana zaidi.

“Ili kufanikisha mdahalo huo ambao ukumbi utakaofanyika utatangazwa hivi karibuni, Taswa imeunda Kamati ya watu sita kusimamia ambao ni Frank Sanga (Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi), Juma Pinto (Mwenyekiti TASWA) na Asha Muhaji (Mhariri wa michezo gazeti la Rai)… Wengine ni Florian Kaijage (Mhariri Mipango Azam TV), Amir Mhando (Mhariri gazeti la Spotileo/Katibu Mkuu TASWA) na Shija Richard (Mhazini Mkuu TASWA),” ilisomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Amir Mhando.

Mhando alisema kwenye taarifa hiyo, mapendekezo ya awali kuhusu washiriki wa kongamano hilo inatarajiwa lihusishe wataalamu kwenye sekta ya michezo, wahariri wa habari za michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Wengine ni wanasheria, wataalamu wa masuala ya hisa, viongozi wa klabu hizo na baadhi ya wadau muhimu wa soka nchini, wakiwemo viongozi wa soka wa zamani katika ngazi mbalimbali.

“Hata hivyo, kikao cha kamati hiyo kitakachofanyika kesho (leo) kitaandaa utaratibu mzima wa kongamano hilo, ikiwemo kupanga waalikwa na namna ya uendeshaji utakavyokuwa na lengo pia liwe ‘live’ katika televisheni ili wadau wengi zaidi wafuatilie,” alisema Mhando.

CHANZO: HABARILEO
Ungana na Soka24 Facebook, Bonyeza  HAPA

0 comments:

Post a Comment