Shirikisho la mpira wa miguu Afrika (CAF), limemthibitisha beki Hassan Kessy kuichezea Yanga katika michuano ya Kombe la CAF CC katika hatua ya makundi.
Caf pia imetuma leseni ya wachezaji wengine watatu wa Yanga walioongezwa kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo, ambao ni Beno Kakolanya, Juma Mahadhi na Andrew Vicent.
Hayo yamethibitishwa na Ofisa habari wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Alfred Licas ambaye amesema kuwa tayari leseni hizo zimetoka kwa ajili ya wachezaji hao kuanza kuitumikia klabu yao siku ya jumapili itakapocheza na MO Bejaia.
"Ni kweli tumepokea leseni za wachezaji wanne wa Yanga walioongezwa katika hatua hii, hivyo wote wapo huru kucheza michuano ya kimataifa kuanzia sasa." alisema Lucas.
Aidha kocha wa Yanga Hans Van Pluijm amesema alikuwa na kikao na wachezaji wake leo asubuhi kuwaonyesha mikanda ya video za MO Bejaia katika kubaini mapungufu yao ili wao wayatumie kupata matokeo katika mchezo wao.
"Asubuhi hii tulifanya kikkao ambapo tuliwaonyesha wachezaji wetu baadhi ya mikanda ya video ya mechi za MO Bejaia. Hivyo wanajua nini watarajie kwa wapinzani wao. " alisema Pluijm.
Yanga ilitinga hatua hii ya makundi baada ya kuiondosha Sagrada Esperanca ya nchini Angola na baadae baada ya Droo ya hatua hii kufanyika ndipo Yanga walipangwa kundi moja na timu za MO Bejaia ya Algeria, TP- Mazembe ya Congo DRC pamoja na Medeama ya nchini Ghana, na itaanza mechi yake ya kwanza dhidi ya MO Bejaia siku ya jumapili juni 19.
0 comments:
Post a Comment