Friday, June 24, 2016

CAF YAIBEBA YANGA KUELEKEA MECHI NA MAZEMBE

Shirikisho la Mpira wa miguu barani Afrika CAF, limewaidhinisha wachezaji watatu wa Yanga ambao walikuwa wanatumikia adhabu ya kadi kucheza, kucheza katika mchezo wao na TP Mazembe.

Wachezaji wa Yanga, Oscar Joshua, Nadir Haroub "Cannavaro" na Deogratius Munish 'Dida' wameruhusiwa na CAF kucheza katika mchezo wao na Mazembe licha ya kuwa na adhabu ya kadi walizozipata katika michezo mbalimbali.
Awali kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda wachezaji hao wasicheze mchezo huo kutokana na kadi hizo.

Dida inasemekana alipewa kadi ya njano kwenye mechi dhidi ya Sagrada Esperanca na akapewa tena kadi nyingine ya njano kwenye mchezo wa juzi waliocheza dhidi ya MO Bejaia, Cannavaro alipewa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Sagrada Esperanca, mchezo ambao Yanga walifanikiwa kusonga mbele kwa jumla ya magoli 2 - 1.

Menejaj wa Yanga, Hafidhi Saleh, amelielezea suala hilo kwa kusema, wamelazimika kutafuta ufafanuzi CAF ili kujua kama wachezaji hao wanaweza kutumika katika mchezo na TP Mazembe, lakini katika barua ambayo CAF wamewajibu Yanga inasema kuwa wachezaji ambao hawaruhusiwi kucheza katika mchezo huo ni Amissi Tambwe na Haji Mwinyi tu na kwamba wengine wote walishamaliza kuzitumikia adhabu zao.

"CAF wameshatutumia barua pepe (Email) na kutuambia wachezaji watakaokosa mechi ya TP Mazembe ni Mwinyi na Tambwe tu, wengine wote hawana tatizo" alisema Saleh.

Yanga iliomba kwa TFF kuiandikia barua CAF kuomba mchezo huo ufanyike Juni 29 saa 1 na nusu usiku badala ya Juni 28 saa 10:00 alasiri, lakini kutokana na ubovu wa jenereta la uwanja wa Taifa ambapo mechi hiyo itachezwa, mchezo huo utachezwa siku ya Jumanne Juni 28 saa 10 jioni. Huo ni mchezo wa pili kwa Yanga katika kundi A na mchezo wa kwanza walipoteza kwa kufungwa goli 1 - 0 na MO Bejaia ya Algeria.

Msimamo wa kundi hilo hadi sasa ni kwamba TP Mazembe ndio wanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na alama tatu na magoli matatu ya kufunga na moja la kufungwa, MO Bejaia nafasi ya pili wakiwa na alama tatu na goli moja, Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa haina alama yoyote huku wakiwa wamefungwa goli moja na Medeama inashika nafasi ya mwisho ikiwa haina alama na huku ikiwa imeruhusu kufungwa magoli matatu wao wakiwa na moja la kufunga.

Bonyeza Hapa Ku-Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook

0 comments:

Post a Comment