Kombe la Europa League limefikia tamati jana kwa mechi ya fainali iliyowakutanisha Liverpool ya nchini Uingereza na Sevilla kutoka Hispania. Fainali hii ilikuwa ni ya tatu mfululizo kwa Sevilla, ambao walishinda fainali zote mbili za misimu miwili iliyopita na jana tena wamefanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo. Liverpool walikuwa wanapewa nafasi kubwa sana ya kubeba taji hilo kutokana na ukame wa vikombe unaoikabili klabu hiyo huku pia ikidhaniwa Sevilla wao wangeingia katika fainali hiyo wakiwa tayari kwa lolote ambalo lingetokea kutokana na kuchukua taji hilo mara 2 mfululizo. Lakini hali ilikuwa ya tofauti na ilivyotarajiwa na wengi baada ya dakika 90 za mchezo huo kumalizika Liverpool ikikubali kipigo cha magoli 3 - 1.
Daniel Sturridge ndiye alikuwa wa kwanza kuipatika Liverpool goli la kuongoza katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza na kuleta matumaini makubwa kwa maelfu ya mashabiki wa Liverpool waliokuwa wanafuatilia mtanange huo. Hadi timu zinakwenda mapumziko Liverpool ilikuwa mbele kwa goli hilo moja.
Lakini mambo yalikuja kubadilika kilipoanza kipindi cha pili kwani dakika ya 46 tu ya mchezo Sevilla walisawazisha goli hilo kupitia kwa Kevin Gameiro akifunga goli lake la 29 katika mashindano yote msimu huu. Goli hilo liliwarudisha Sevilla katika mchezo na kuwapoteza Liverpool ambao waliruhusu tena goli katika dakika ya 64 lililofungwa na Coke, hali iliyoongeza presha zaidi kwa wachezaji na kocha wa Liverpool na kuona kila dalili la jahazi lao kuzama, huku Sevilla nao wakizidi kulisakama lango la Liverpool licha ya kuwa wako mbele kwa magoli 2 - 1. Dakika ya 70 Coke alizidi kuzima ndoto za Liverpool kuchukua ubingwa huo pale alipoifungia timu yake goli la 3 na kuifanya Sevilla kuwa mbele kwa magoli 3 - 1. Hadi mwamuzi anapuliza kipyenga cha mwisho Liverpool 1 - 3 Sevilla.
Huu unakuwa ubingwa wa 3 mfululizo wa kombe la Europa kwa klabu ya Sevilla baada ya kuchukua katika msimu wa 2013-14. 2014-15 na 2015-16. Na sasa watashiriki michuano ya klabu Bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League Msimu ujao.
Baada ya mechi hiyo Kocha wa Liverpool aliwaahidi mashabiki wa Liverpool kuwa watajipanga ili waweze kufanya vizuri huku akisema yeye ndo anahusika na matokeo ya mchezo huo hivyo kuwataka mashabiki kuwa watulivu huku akisisitiza kuwa Liverpool itarudi upya ikiwa iko fiti 100%
0 comments:
Post a Comment