Wednesday, December 28, 2016

YA LWANDAMINA NA KIBARUA CHAKE YANGA

Kocha Mkuu wa Yanga George Lwandamina amesema kazi ya ukocha inahitaji uwepo wa kikosi chenye vipaji tofauti na uwezo husika. Lwandamina aliyejiunga na Yanga akitokea Zesco ya nchini Zambia, tangu kutua kwake mashabiki na wapenzi mbalimbali wa Yanga wamekuwa na matumaini makubwa juu ya klabu yao kufanya vizuri katika michuano ya ndani na hata ile ya kimataifa kutokana na historia nzuri ya kocha huyo.

Hadi Sasa Lwandamina ameiongoza Yanga katika michezo mitatu,  miwili ya Ligi na mmoja wa kirafiki, na kufanikiwa kushinda mechi moja kati ya hizo tatu, huku akipoteza mchezo mmoja dhidi ya JKU na nyingine kutoa sare na klabu ya African Lyon.

"Kuongoza ama kusimamia timu ya mpira wa miguu inahitaji mseto wenye vipaji tofauti na ujuzi wa mchezo husika. Sambamba na mbinu mbalimbali, Makocha wawe na uwezo wa kushirikiana binafsi na wachezaji kuwahamasisha na kuwajengea misingi ya nidhamu. Mafunzo yao hupaswa kupokelewa ipasavyo na lazima yaendane na hali za wachezaji kiakili na kimwili, Kitu maalum na cha msingi ni uwezo wa kocha kufanya mabadiliko yenye tija na kimbinu wakati wa mchezo.
" alisema.

Kocha huyo aliongeza kuwa cha muhimu zaidi kama kocha ni heshima kutoka kwa wachezaji wake kwa kuwasimamia kiuweledi ili kuweza kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.

"Muhimu zaidi , makocha huitaji heshima kutoka kwa wachezaji wake kwa kuwaongoza kiuweledi. Wakufunzi wengi waliobobea kimbinu hushindwa kutokana na wao kushindwa kuongoza. Inahitaji mtu maalum kuweza kuwa Msanii pia mkufunzi jeshini"

Yanga leo inashuka dimbani kumenyana na Ndanda FC katika mchezo wa tatu wa raundi ya pili ya ligi kuu Tanzania bara, ikiwa pia ni mechi ya nne kwa kocha Lwandamina kuiongoza Yanga tangu alipojiunga nayo akitokea Zesco United ya Zambia.

0 comments:

Post a Comment