Monday, July 11, 2016

JERRY MURO ATAKIWA KUWA NA ADABU

Sakata la Ofisa habari wa Yanga Jerry Muro kufungiwa mwaka mmoja kutojihusisha na maswala ya soka pamoja na kupigwa faini ya sh. Milioni tatu limechukua sura mpya baada ya viongozi wa TFF kujibu kauli za Msemaji huyo.
Katibu Mkuu Wa TFF, Selestine Mwesigwa

Suala hilo limechukua sura mpya baada ya TFF kumtaka Jerry Muro kuwa na adabu huku wakisema kuwa adabu hainunuliwi dukani. Hayo yamesemwa na katibu mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kufuatia kauli za Jerry Muro kuwa TFF imekurupuka na kwamba haizingatia haki za kibinadamu wakati wakitoa adhabu hiyo.

kwa upande mwingine Ofisa habari wa shirikisho hilo, Alfred Lucas ameonyesha kushangazwa na kauli kali anazozitoa Jerry Muro huku akisema kuwa TFF imeshafunga mjadala wa suala hilo.

"Hukumu ishatoka, alishapewa nakala ya hukumu yake, yeye kama anaendelea kutoa lugha za kukashifu, muache aendelee sisi kwa upande wa TFF tulishalifunga suala hilo" alisema Lucas.

Viongozi wa TFF wameamua kutoa kauli hizo kwa kile kilichodaiwa na Jerry Muro kuwa yeye ana akili nyingi zaidi kuliko viongozi wa TFF na kutaka wasimsumbue kwa kuwa yeye si mwanachama wa TFF.
Ofisa habari huyo wa Yanga alienda mbali zaidi na kuanza kuhoji elimu ya viongozi hao wa TFF.

Hata hivyo, pamoja na Muro kudai kuwa yeye ni muajiriwa na si mwanachama wa TFF, Yanga ni mwanachama wa Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), CAF, FIFA na TFF, yeyote kiongozi wa Yanga anaweza kuadhibiwa na mashirikisho hayo kwa kuwa msemaji wa klabu ni agizo la Fifa ambalo lipo ndani ya katiba za wanachama wake na wanachama wa shirikisho husika.
Bonyeza Hapa Ku-Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook

0 comments:

Post a Comment