Saturday, May 21, 2016

SAKATA LA STAND UNITED KUWA KAMPUNI LAZIDI KULETA UTATA

Wanachama na Mashabiki wa klabu ya Stand United Wamepinga suala ya timu yao kuendeshwa kama kampuni.




Siku Chache zilizopita Soka24 ilikuletea taarifa juu ya kampuni ya ACACIA inayoidhamini klabu ya Stand United kutishia kuondoa udhamini wao endapo klabu hiyo itaendeshwa kwa misingi ya kampuni huku mwenyekiti wa klabu hiyo Amani Vicent akikiri kupokea barua kutoka kwa ACACIA iliyoeleza tishio la kujitoa kwao. Hali imezidi kuwa tete klabuni hapo baada ya jana mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuitisha mkutano kupinga maamuzi hayo ya kuifanya Stand  kuendeshwa kama Kampuni.

Wakizungumza jana mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, wameonyesha kukerwa na kusikitishwa sana na maamuzi hayo huku wakisema ni kuipoteza timu na kuhatarisha udhamini wao na ACACIA. Walipoulizwa kuhusu wanachama 52 wenyewe ndo wameonekana kuridhia maamuzi ya Stand kuwa Kampuni,  walisema sio kweli kwani Stand ina zaidi ya Wanachama 100 na kwamba hao 52 wanaosemwa ni kikundi tu kinachoongozwa na Amani Vicent lengo likiwa ni kuihujumu timu na kufanya vile wao wanavyotaka.

Stand United ilipata udhamini mnono kutoka kwa ACACIA na familia ya soka Tanzania iliamini kuwa udhamini huo utaleta mafanikio makubwa katika klabu hiyo lakini mambo yamekuwa tofauti na yalivyokatarajiwa kwani migogoro klabuni hapo inazidi kushamiri siku hadi siku.

Stand wanachezea shilingi chooni na muda si mrefu shilingi hiyo itadumbukia shimoni. 

0 comments:

Post a Comment