Farid Mussa, amesema kuwa hivi sasa yupo fiti kukabiliana na changamoto ya soka la Hispania endapo atajiunga na Club Deportivo Tenerife msimu ujao.
Farid aliyerejea nchini jana akitokea katika timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Hispania ‘Segunda Division’, amefuzu majaribio kujiunga na timu hiyo na kinachosubiriwa hivi sasa ni kumalizika kwa mazungumzo baina ya viongozi wa Azam FC na timu hiyo iliyoonyesha nia kubwa ya kumsajili winga huyo baada ya kuridhishwa naye kwa kipindi cha mwezi mmoja alichotumia kwa majaribio hayo.
Farid amesema kuwa amekutana na changamoto nyingi sana alipokuwa kwenye majaribio ndani ya kikosi hicho hadi kufuzu, lakini hivi sasa ameshazizoea na yupo tayari kwa mapambano endapo atajiunga nayo kwa msimu ujao.
“Kwanza kule nimekutana na hali ya hewa na mandhari tofauti na hapa, pia vyakula navyo ni tofauti sana hivyo ilinichukua muda kuzoea mambo yote hayo, hata mfumo wa uchezaji na mazoezi ya wenzetu ni tofauti sana, mwanzo ilinipa shida sana lakini hivi sasa nimezoea na kuona ni kawaida sana.
“Hata wenyewe walinishangaa sana kwa namna nilivyozoea haraka na nilivyokuwa nacheza, naweza kusema nipo fiti hivi sasa kupambana na changamoto zote kule,” alisema.
“Najisikia vizuri sana kufuzu majaribio na namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa hatua niliyofika, watu wa kule Hispania wameonyesha kunikubali sana na najivunia kwa hilo kiukweli nimefurahishwa na hilo sana, kwa hiyo mimi ni juhudi tu nitakazoziongeza kwenye mazoezi kwani malengo ninayoyataka mimi na sehemu ninayotaka nifike bado sana na ndio maana napambana sana niwezavyo,” alimalizia.
Farid aliyekuzwa kwenye kituo cha kulelea vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’, hadi anapata nafasi hiyo ya kwenda Hispania kwa kiasi fulani imechangiwa na kiwango chake bora msimu huu baada ya kuchezeshwa mara kwa mara katika kikosi cha timu kubwa.
0 comments:
Post a Comment