KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Dennis Kitambi, amesema kuwa maelekezo waliyowapa wachezaji wao ya kuongeza hali ya kupambana mchezoni kabla ya kuanza kipindi cha pili ndio yamepelekea kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 jana jioni dhidi ya Majimaji ya Songea.
Kitambi amesema pia mabadiliko waliyofanya ya kumwingiza mshambuliaji Ame Ally kipindi cha pili na kumpumzisha Didier Kavumbagu, nayo yamechangia kuondoka na pointi tatu zote katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
“Kwanza nianze kwa kuwapongeza Majimaji kwani walifanikiwa kutukaba kuanzia juu kipindi cha kwanza, walicheza vizuri na awali tulijua kabisa kuwa watakuja na hali ya juu ya kupambana katika mchezo huu, kwa upande wetu sisi kipindi cha kwanza kujituma kwetu hakukuridhisha kwa hiyo hilo lilitufanya tusiweze kufanya vizuri, mapumziko tukaongelea hilo na tukafanya mabadiliko.
“Wachezaji tuliwapa maelekezo ya kuwa tunahitaji hali ya kupambana zaidi kwa sababu kipindi cha kwanza wachezaji wa Majimaji walipambana kupita sisi, kwa hiyo tulivyorudi kipindi cha pili tukapata mabao hayo kupitia kwa Mudathir (Yahya) na tulijua kabisa Majimaji wakirudi kipindi cha pili watashindwa kucheza kwa hali ile ile kwani watakuwa wamechoka,” alisema Kitambi mara baada ya mchezo huo.
Kuwakosa nyota kumi
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, iliingia katika mchezo huo ikiwakosa wachezaji wake 10 Pascal Wawa, Shomari Kapombe, Wazir Salum, Racine Diouf, Michael Bolou, Frank Domayo, Allan Wanga, Kipre Tchetche, ambao ni wagonjwa Farid Mussa akiwa majaribioni nchini Hispania huku Himid Mao akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata dhidi ya Mtibwa Sugar.
Akizungumzia mapengo hayo yamewaathiri kiasi gani, Kitambi alisema kwa kiasi fulani imewaathiri lakini amedai kuwa ni fursa kwa wachezaji waliokuwa hawapati nafasi kucheza na kuonyesha uwezo wao.
“Kama umeona leo (jana) Mudathir ametumia vema nafasi hiyo kwa kutupa mabao mawili ya ushindi, ndio inatuathiri kwani tulikuwa na upungufu wa watu 10 wa kuchagua katika mchezo huo, lakini suala hili la majeruhi litaendelea kuwepo hivyo ni lazima tutafute mbinu ya kuwatumia wachezaji waliopo na naamini wanaweza kufanya vizuri kama Muda leo alivyodhihirisha,” alisema.
Azam FC leo asubuhi imeendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Simba, utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili ijayo Mei Mosi.
Source: Azam Fc Official site
Pata habari za michezo kwa haraka zaidi kupitia soka24.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment