Saturday, April 16, 2016

Azam Fc Kuifuata Esperance De Tunis


KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuondoka leo kuelekea jijini Tunis kwa ajili ya kukabiliana na Esperance ya huko kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika katika Uwanja wa Olympique de Rades Jumanne ijayo Aprili 19.

Azam FC inaelekea jijini humo ikiwa na kikosi kamili, na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita, yaliyofungwa na Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, alisema wako vizuri kimbinu na wanajua namna ya kuukabili mchezo huo unaotarajia kuwa na upinzani mkubwa.

“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri, kila mmoja anafanya kazi kwa bidii, Erasto Nyoni na John Bocco wamerejea kwenye mazoezi, hivyo tunafanya kazi nguvu kwenye mazoezi yetu kwa ajili ya mchezo huo,” alisema.

“Tunacheza na timu inayoshika nafasi ya tatu Afrika kwa mujibu wa viwango vya CAF vilivyotoka sisi tukiwa namba 345 hivyo lazima watu watambue hilo, tuna nafasi ya kuendeleza mazuri tuliyofanya hapa na nafasi yetu nzuri ya kusonga mbele jijini Tunis ni kufunga bao la ugenini, hivyo lazima tufanya kazi ya ziada kutimiza hilo na kimbinu tuko vizuri,” alimalizia Hall.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB inahitaji sare yoyote au ushindi ili iweze kusonga mbele kwa hatua ya 16 bora (play off), itakapokutana na moja ya timu iliyotoka kwenye hatua hiyo ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikifuzu hapo itatinga moja kwa moja katika hatua ya makundi ya michuano hiyo (robo fainali).

Kikosi cha Azam FC kinaondoka kikiwa kimefanya mazoezi leo asubuhi na mara kitakapowasili kesho jijini Tunis kinatarajia kuangalia kitu cha kufanya kabla ya keshokutwa kufanya mazoezi katika uwanja utakaofanyika mchezo huo.  

chanzo: Azam Fc Official Site 

0 comments:

Post a Comment