Saturday, July 9, 2016

JERRY MURO: "TFF IMETANGA VITA NA YANGA"

Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro amepinga vikali maamuzi ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF, kwa kudai kuwa haitambui adhabu hiyo na kwamba yeye ataendelea kufanya kazi.

TFF imetoa adhabu ya kumfungia Jerry Muro mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya Soka kwa kile kilichodaiwa na TFF kuwa Ofisa Habari huyo wa Yanga alikuwa anatoa kauli za uchochezi zilizosababisha vurugu kati ya mashabiki wa Simba na Yanga mwaka jana pamoja na kususia vikao alivyokuwa anaitwa na TFF ili kwenda kujieleza, wakati huo Jerry yeye amesema TFF sio waajiri wake hivyo hawana mamlaka ya kumfungia kwa kuwa yeye ni muajiriwa na si mwanachama wa TFF.

"Sikubaliani na Hukumu, isitoshe TFF wamekiuka misingi ya haki za kibinadamu hawajanipa nafasi ya kujitetea, kesi imesikilizwa upande mmoja, sikubaliani na hilo" alisema Muro.

Hata hivyo TFF walipeleka barua makao makuu ya Yanga, wakamkuta katibu ambaye aliwajulisha kuwa Jerry Muro ameanza likizo tangu julai mosi na yupo kijijini kwao Machame.

"Eti wanasema nimekiuka matakwa ya TFF, mimi sio muajiriwa wa TFF sipaswi kutekeleza matakwa ya TFF, napaswa kutekeleza ya Yanga, mimi sio kiongozi wa Yanga ni muajiriwa tu, viongozi wa Yanga wakiniambia Jerry kaa pembeni nitakaa lakini sio TFF, nitaendelea kuongelea mambo ya Yanga yangu kama kawaida na kwa kitendo hiki TFF imetangaza vita na Yanga" aliongeza Ofisa Habari Huyo.


Kwa mujibu wa kanuni ya 35 za soka za TFF inayozungumzia udhibiti wa viongozi inasema, kiongozi akitoa matamshi au ishara za matusi dhidi ya mashabiki, akitoa matamshi, ishara za matusi yenye nia ya kumdhalilisha kiongozi mbele ya jamii awe wa TFF, klabu au Taifa atatozwa faini ya Sh milioni 1 (1,000,000/=) na/au kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6) au vyote kwa pamoja.

(i) Ni marufuku kwa kiongozi wa klabu kushutumu au kutoa matamshi yenye lengo la kumkashifu au kumdhalilisha kiongozi wa TFF/Chama cha Mpira cha ngazi husika kwenye vyombo vya habari. (j) Hairuhusiwi kwa kiongozi au Klabu kutoa matamshi au kuzungumzia jambo lolote linalohusu TFF kwenye vyombo vya habari bila ya kuwasiliana.

(m) Pamoja na adhabu zilizoainishwa kwenye Kanuni hii, TFF inaweza kutoa adhabu nyingine kwa kuongeza au kupunguza ikiona kuna ulazima.

Makosa anayotuhumiwa nayo Jerry ni pamoja na kukashifu, kuipinga na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari hukumu ambayo imeridhiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ambaye ndiye aliyewasilisha malalamiko ya TFF kwenye kamati ya maadili akiwa kama mtendaji mkuu wa shirikisho hilo.

Hii inakuwa ni adhabu ya pili kwa Muro baada ya Mei 5 mwaka jana, Kamati ya Nidhamu ya TFF ilimpiga faini ya Sh 5 milioni kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.
Bonyeza Hapa Ku-Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook

0 comments:

Post a Comment