Tuesday, April 26, 2016

Farid Mussa Aanza Majaribio La Liga


WINGA machachari wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Farid Mussa, ameanza majaribio rasmi nchini Hispania akiwa na kikosi cha timu ya CD Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.

Farid, 20, aliyefika juzi nchini humo akitokea Tunisia, Azam FC ilipokwenda kucheza na Esperance ya huko kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo usiku wa kuamkia leo alitarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa Tenerife watakaocheza mchezo wa kirafiki na moja ya timu ya Ligi Daraja la Kwanza huko.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kutoka nchini humo Farid alisema benchi la ufundi la Tenerife lilipanga kumpa dakika 45 za kucheza ili kuonyesha uwezo wake kwenye mchezo huo ikiwa ni sehemu ya majaribio pia.

“Namshukuru Mungu wamenipokea vizuri na wameonyesha kunikubali, kiufupi naendelea vizuri sana huku na usiku wa leo (jana) nitaanza kwa kucheza mchezo wa kirafiki kwa dakika 45, nimejipanga kufanya vema katika sehemu yangu ya majaribio huku ili niweze kubakia huku na kuitangaza timu yangu ya Azam FC,” alisema.

Nyota huyo chipukizi aliyekuzwa na kituo cha kulea vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’, alimalizia kwa kusema kuwa kwa mujibu wa wakala wake John Sorzano raia wa Venezuela aliyeishi sana nchini England, amedai kuwa wiki ijayo anatarajia kuanza rasmi majaribio katika timu mbili za Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ akianzia Las Palmas na kumalizia Malaga.

Farid atafanya majaribio hayo na kukaa huko kwa takribani wiki tatu na anatarajia kurejea nchini Mei 19 mwaka huu, hiyo inamaanisha kuwa atakosa mechi zote za Azam FC zilizobakia za msimu huu.

Lakini mechi pekee ambayo anaweza kuiwahi ni ile ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayofanyika Mei 25 mwaka huu, ambayo Azam FC ilitinga juzi kwa kuichapa Mwadui ya Shinyanga na itacheza na mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya Yanga na Coastal Union.   

Chanzo: Azam Fc Official Site




Pata habari za michezo kwa haraka zaidi kupitia soka24.blogspot.com

0 comments:

Post a Comment