Friday, June 24, 2016

KOCHA MPYA SIMBA APEWA RUNGU LA KUSAJILI WAKIMATAIFA

Simba ipo mbioni kukamilisha usajili wa kocha Joseph Omog na tayari imeshampa ruksa kocha huyo kusajili wachezaji wakimataifa.

Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba ni kwamba kocha huyo anatarajiwa kutua muda wowote kuanzia hivi sasa kujiunga na klabu hiyo pamoja na kuanza rasmi kukinoa kikosi hicho.
Taarifa hizo zinasema kwamba kama kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa na kocha huyo kukabidhiwa jukumu la kukinoa kikosi hicho, atafanya kazi na kamati ya usajili ya klabu hiyo, kamati ambayo ipo chini ya uongozi wa Zacharia Hans Poppe.

"Kuna wachezaji wengi wamekuja kwa ajili ya majaribio, kuna wengine wameonekana nchi mbalimbali hivyo nao watakuja hapa nchini na kucheza mechi mbili za kirafiki chini ya Omog ambaye atawaangalia na kuona yupi anafaa kuvaa jezi za Simba msimu ujao" alisema Mtoa habari huyo.

Kwa upande mwingine kocha Omog ameweka wazi kuwa mazungumzo na klabu ya Simba yanaendelea vizuri na kwamba muda wowote atarejea nchini.

"Kila kitu kipo vizuri, ninachosubiri ni tiketi kutoka Simba, muda wowote kuanzia sasa nitakuja Tanzania kuifundisha Simba" alisema Omog alipozungumza na Gazeti la michezo la Bingwa.

Katika orodha ya makocha ambao Simba walihitaji kuwasajili, Omog alikuwa ni chaguo la tatu hata hivyo kutokana na rekodi zake nzuri katika soka Simba imeona sio vibaya kama watampa timu yao kwani wanaamini ataifikisha wanapopataka.

Dili ambazo zimefeli ni ile ya Kocha Mghana Sellas Tetteh ambaye aliwaambia Simba kama wanamtaka basi wamsubiri hadi amalize kuifundisha Sierra Leone kwenye mechi ya mwisho ya kufuzu Afcon wakati kocha Mzimbabwe Kalisto Pasuwa alibadili uamuzi wake wa kujiunga na Simba baada ya kuiwezesha Zimbabwe kufuzu Afcon.

Like Ukurasa Wa Soka24 Facebook Hapa

0 comments:

Post a Comment